Wednesday, 8 June 2016

WABUNGE UKAWA SASA KUKATWA POSHO

HATIMAYE bunge limetoa uamuzi wa kuwakata posho wabunge wa kambi ya upinzani (UKAWA), kwa muda wote ambao hawajahudhuria vikao vya bunge bila sababu za msingi.

Uamuzi huo ulitangazwa bungeni mjini hapa jana, muda mfupi baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Filip Mpango, kumaliza kusoma bajeti ya serikali ya mwaka 2016/17.

Akitangaza uamuzi huo, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alisema wametafakari kwa kina mwenendo wa wabunge hao kusaini posho bila kuhudhuria vikao na kutekeleza majukumu yao ya kibunge na kuamua kufikia uamuzi huo.

“Wabunge wa vyama vya upinzani, ambao wanatoka nje na kuacha kufanya mijadala ndani ya bunge, hawatalipwa posho zao kwa siku zote ambazo wametoka nje,”alisema.

Alisema baada ya kupokea miongozo mbalimbali, ametafakari kwa kina na kuona kuwa, wabunge hao hawapaswi kulipwa posho hizo za vikao kwa kuwa ni kinyume na taratibu.

Kutokana na hali hiyo, Naibu Spika alilazimika kutoa ufafanuzi wa miongozo mbalimbali, ambayo imekuwa ikitolewa na wabunge kuhusu baadhi ya wabunge kutoshiriki vikao na kupokea posho.

Wabunge hao wa upinzani kwa takriban wiki mbili, wamesusia vikao vya bunge, ambapo wamekuwa wakipishana na Naibu Spika kila anapoingia kwa ajili ya kuongoza shughuli za bunge kwa madai hawana imani naye.

Wabunge hao wameendeleza mtindo huo, ambapo jana walisusia hotuba ya bajeti kuu ya serikali baada ya kikao hicho kuongozwa na Naibu Spika, ambapo walitoka nje baada ya kiongozi huyo kukaa kitini na kuwaamuru wabunge waketi.

No comments:

Post a Comment