Wednesday, 8 June 2016
POLISI WAPIGA MARUFUKU MIKUTANO NA MAANDAMANO YA UKAWA
SIKU chache baada ya Muungano wa Vyama vya Upinzani (UKAWA), kutangaza kuzunguuka nchi nzima kuishitaki serikali ya awamu ya tano kwa wananchi, Jeshi la Polisi limepiga marufuku mikutano na maandamano yote ya kisiasa nchi nzima.
Jeshi hilo limesema mikutano na maandamano hayo yana viashiria vya uvunjifu wa amani kwa kuwa yanataka kuwahamasisha wananchi kutotii sheria za nchi.
Aidha, polisi imemuonya mtu yeyote atakayekaidi amri hiyo kwa kusema atakiona cha moto kwa kuwa hataachwa bila kuchukuliwa hatua.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam, jana, Kamishna wa Polisi, Operesheni na Mafunzo kutoka Makao Makuu, Nsato Mssanzya, alisema jeshi hilo limepata taarifa za kiintelejensia kwamba, mikutano na maandamano hayo hayana nia njema, hivyo hayawezi kuachwa yaendelee.
"Katika siku za karibuni, Jeshi la Polisi nchini limepokea taarifa kutoka kwa baadhi ya vyama vya siasa vikitaka kufanya mikutano na maandamano. Hata hivyo, kupitia vyanzo vyake mbalimbali, limebaini kuwa mikutano hiyo ina lengo la kuwahamasisha wananchi kutotii sheria za nchi (civil disorder).
"Aidha, vyama vingine vya siasa vimeonyesha dhamira ya kupinga kile ambacho kitasemwa na wapinzani wao. Vyanzo hivyo vimebainisha kwamba, upo uwezekano mkubwa wa kutokea vurugu baina ya makundi mawili ya kisiasa,"alisema.
Kwa mujibu wa Kamishna Nsato, Jeshi la Polisi linapiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara kuanzia jana, hadi pale hali ya usalama itakapotengemaa na kwamba, limewataka wanasiasa kuacha mara moja kuwashinikiza wananchi kutotii sheria za nchi.
Alisema polisi haitasita kumchukulia hatua kali za kisheria mtu au chama chochote cha siasa kitakachokaidi agizo hilo.
Kamishna huyo pia aliwataka wananchi kuwa makini na wanasiasa wenye lengo la kutaka kuvuruga amani ya nchi na kwamba, anawasihi waendelee kushirikiana katika kujenga umoja na mshikamano wa nchi.
UKAWA, kupitia viongozi wake mbalimbali, walipanga kuzunguuka maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuishitaki serikali kwa wananchi, kwa kile ilichodai ukiukwaji wa sheria na taratibu, unaofanywa na serikali, ikiwemo operesheni ya kuwatumbua majipu watendaji wasiowajibika ipasavyo na wale wanaotuhumiwa kwa mambo mbalimbali, ambao huwekwa pembeni ili kupisha uchunguzi.
Kutokana na mpango huo wa UKAWA, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia msemaji wake, Christopher Ole Sendeka, kilisema haitakaa kimya na kuwatazama wapinzani wakipotosha mambo, badala yake kitakwenda nao hatua kwa hatua ili kujibu kila tuhuma na uongo utakaokuwa ukisambazwa dhidi ya serikali na viongozi wake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment