Tuesday 12 April 2016

OLE SENDEKA ATEMA CHECHE





CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeitaka serikali ya awamu ya tano, kuendelea kuwasaka watumishi hewa walioisababishia hasara kubwa ili wachukuliwe hatua, ikiwemo kuwaamuru walipe fedha hizo zifanye kazi zingine kwa manufaa ya wengi.
Kimesema kitaendelea kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli katika jitihada zake za kuwaletea Watanzania maisha bora kwa kuwabana wabadhirifu, wezi wa mali za umma na hakitakaa kimya atakapojitokeza mtu wa kumzuia.
Kimesema viongozi wa juu wa CCM watazunguka nchi nzima kuhakikisha watendaji wa ngazi zote katika Chama, wanafanya kazi ya kuwatumikia wananchi kwa uadilifu kama inavyoeleza misingi ya CCM pamoja na kukagua utekelezaji wa Ilani.
Pia, kimesema hakitakaa kimya kuangalia wachache wakidhulumu haki za Watanzania kwa sababu kimeingia nao mkataba wa kuwatumikia kwa miaka mitano kupitia Ilani hiyo ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.
Akizungumza jana, wilayani Babati, mkoani Manyara, kwenye mkutano wa kwanza wa hadhara, Msemaji Mkuu wa CCM Taifa, Christopher Ole Sendeka, alisema CCM imepewa dhamana na Watanzania kuiongoza nchi na itafanya hivyo bila kuchoka.
Alisema tangu kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya tano, inayoogozwa na CCM, tayari mambo makubwa yamefanyika na bado yataendelea kufanywa kwa nguvu zote na kwamba kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ inafanywa na Rais Magufuli kwa vitendo.
Ole Sendeka alisema CCM inatuma salamu kwa baadhi ya watu wanaoendelea kueneza siasa ya chuki, dharau, matusi kama ile ya wakati wa uchaguzi mkuu kwamba, waache kwa sababu hawana nafasi kwa serikali ya awamu hii, iliyokusudia kuwatumikia Watanzania bila ubaguzi wa kiitikadi.
"CCM ni ya Watanzania, tunaanza zoezi la nchi nchi nzima kuwaeleza wananchi kuwa yapo maisha baada ya uchaguzi, ambayo ndio CCM tunayaishi sasa. Tunachapa kazi kama tulivyoahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi na tutaendelea kufanya hivyo, wanaokosoa utendaji wetu si wazalendo," alisema.
Aidha, alisema urais wa Dk. Magufuli hauna ubia na kiongozi yeyote wa nchi hii na kwamba, anatimiza wajibu wake kwa misingi ya sheria na kanuni za nchi.
Alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania kuendelea kuiunga mkono CCM na serikali yake, ili iendelee kutekeleza majukumu yake kwa umma na wawapuuze wanaokosoa juhudi hizo kwa maslahi binafsi.
Awali, Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa Mkoa wa Kigoma, ambaye aliambatana na Ole Sendeka, kwenye ziara hiyo, Kilumbe Ng'enda, alisema lengo la ziara hiyo ni kuwashukuru wananchi wa Kata ya Bashneti kwa kuichagua CCM baada ya kuwa chini ya upinzani kwa miaka 15 iliyopita.
Katika matokeo ya uchaguzi uliopita, kata hiyo ilimchagua Jovita Mandoo wa CCM kuwa diwani kwa mara ya kwanza, baada ya miaka 15, ambapo tayari ameanza kazi ya kujenga ofisi ya kata.
Katika kuunga mkono juhudi hizo, Ole Sendeka alichangia mabati ili kukamilisha ujenzi huo.
Leo, Ole Sendeka anaendelea na ziara yake mkoani humo kwa kukutana na viogozi wa wilaya na mkoa wa Chama ili kuzungumza nao mambo mbalimbali ya kukiimarisha Chama.

No comments:

Post a Comment