Monday 25 September 2017

SAMIA: RUSHWA INAINYIMA UHURU SEKTA YA MAHAKAMA


MAKAMU wa Rais, Samia Suluh Hassan amesema tatizo la rushwa linanyima uhuru katika sekta ya mahakama, hivyo kuna haja Jumuia ya Madola, kuweka mikakati ya bajeti ili kupunguza changamoto zilizopo.
Amesisitiza kuwepo haja ya sekta hiyo kufichua maovu na kutoa adhabu kali kwa watendaji wanaoichafua taaalamu hiyo kwa vitendo vya rushwa, ufisadi na ukiukaji wa maadili.
Akizungumza jana, jijini Dar es Salaam, katika Mkutano wa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Nchi za Jumuia ya Madola, Samia alisema suala la  rushwa ni mwiba kwenye taaluma hiyo, hivyo wahalifu wanapaswa kufichuliwa.
“Mahakama ndiyo chombo pekee cha kutoa haki. Inapokiuka kwa sababu ya rushwa au ufisadi ni hatari. Imefika wakati kurejesha imani za wananchi katika muhimili huo kwa Jumuiya ya Madola kuhakikisha inafichua maovu yanayojitokeza,”alisema.
Alisema hatua ya changamoto ya ucheleweshaji wa kesi mahakamani na kuwapo kwa mlundikano wa kesi nyingi, ni tatizo, hivyo ipo haja kufanyiwa kazi ipasavyo.
“Kesi inapochelewa kuna vitu vingi, ikiwemo ufinyu wa bajeti au kuchelewa kwa upelelezi, lakini mtu hawezi kuelewa kwa kuwa tayari dhana ya rushwa imetawala katika sekta hiyo. Tujitahidi kufanyakazi kwa ufanisi ili kupunguza migogoro iliyopo,”alisema.
Makamu wa Rais aliongeza kuwa, Tanzania imepiga hatua katika kushughulikia changamoto za mahakama zilizopo, kwa kuhakikisha wanapunguza kesi na kushughulikia zilizopo kwa wakati.
Alisema ni muhimu kuzingatia haki na usawa na kuongeza bajeti ya sekta hiyo ili kuwezesha mahakama kufanyakazi bila kuingiliwa.
“Sekta hii ina changamoto nyingi, ikiwemo ya miundombinu ya majengo yaliyopo kwa kuwa hayatoshi na chakavu. Serikali ya Tanzania imeona haja ya kuwezesha sekta hiyo katika bajeti yake na kupewa fedha kwa wakati ili kupunguza matatizo yaliyopo,”alisema.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamisi Juma, alisema mkutano huo wenye lengo la ushirikiano shirikishi katika sekta ya mahakama, utaibua mikakati ya uwezeshaji wa kufanya kazi kwa ubora na kuzingatia sheria.
Alisema Tanzania imeanza kufikia malengo yake ya kuwezesha sekta hiyo kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, ambapo ujenzi wa majengo ya mahakama kwa bei nafuu bila kutumia tofali umeanza.
Alisema kutokana na hatua hiyo, hadi kufikia mwaka 2020, mahakama 175 za mwanzo, mahakama kuu na mabaraza ya mahakama, ujenzi wake utakuwa umekamilika.
Alisema mkakati wa kuondokana na tuhuma za ufisadi, rushwa na utendaji usioridhisha ni endelevu na kila mmoja anapimwa kwa malengo katika kumaliza changamoto za kesi zilizopo.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania, Ignas Kitusi, alisema  maudhui ya mkutano huo ni kujenga mahakama shirikishi, inayowajibika katika utendaji ili taasisi hiyo ifikie lengo.
Alisema katika mkutano huo, ni lazima kujikosoa na kusemana ukweli na kujadili kwa kina mada zenye kujenga sekta hiyo ili kuwa na utendaji bora.
“Changamoto zinazoikabili sekta ya mahakama kwa nchi zinazoendelea ni ufinyu wa bajeti ndio sababu ya kulega lega kwa huduma,”alisema.
Alisema Tanzania tangu mwaka 2012, imeingia katika mpango wa mageuzi, ambao unalenga kujenga mahakama zenye maslahi ya wananchi kwa kusogeza na kuboresha  huduma kwa kuondoa vikwazo vya kisheria na kiutendaji vilivyokuwa vinachelewesha mashauri.
Tanzania imepewa heshima kwa mara ya kwanza kuwa mwenyeji wa mkutano huo, ambao ni mara ya pili kufanyika kwa nchi za Afrika, ambapo awali  ulifanyika nchini Uganda.

No comments:

Post a Comment