POLISI nchini imesema inaendesha msako mkali kwa
madereva kufuatia kuongezeka kwa ukamataji wa makosa ya ulevi barabarani.
Makosa hayo yameongezeka mpaka kufikia 2,795, sawa
na asilimia 21, katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Julai, mwaka huu.
Pia, polisi wamedhamiria kukomesha tabia za baadhi
ya madereva, kuendesha magari wakiwa wamelewa huku wengine wakisikiliza simu,
jambo ambalo linaweza kusababisha ajali.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Fortunatus
Musilimu, aliliambia gazeti hili hivi karibuni kuwa, dhamira ya polisi ni
kukomesha vitendo hivyo vilivyokithiri kwa madereva.
Alisema watapambana na madereva, ambao wamekuwa
wakishindwa kutii sheria bila shuruti.
Kamanda Musilimu alisema, msako dhidi ya madereva
walevi, unaendelea kufanyika nchi nzima, ambapo tayari yamefanyika makosa
15,988, katika kipindi hicho cha mwaka huu, ikilinganishwa na makosa 13,193,
mwaka jana.
Alisema msako huo umewezesha kupungua kwa ajali za barabarani
2,749, ambazo ni sawa na asilimia 45, kwa kipindi cha Januari hadi Julai, mwaka
huu.
Mwaka jana, ajali hizo zilikuwa 3,354, tofauti na
Januari hadi Julai, mwaka jana, ambapo zilikuwa 6,103.
Pia, alisema wameweza kupunguza ajali zilizokuwa
zinasababisha vifo vya barabarani 468, sawa na asilimia 24, kwa kipindi cha
Januari hadi Julai, mwaka huu.
Alisema katika kipindi hicho, vilitokea vifo 1,477,
ikilinganishwa na kipindi cha Januari hadi Julai, mwaka jana, ambapo
vilitokea vifo 1,945.
Musilimu alisema idadi ya majeruhi kutokana na
ajali za barabarani pia imepungua hadi 2,459, sawa na asilimia 44, kwa kipindi cha
Januari hadi Julai, mwaka huu. Mwaka jana, idadi ya majeruhi ilikuwa 5,656.
Alisema operesheni hiyo pia imewezesha kuongezeka kwa
ukamataji wa makosa 1,597, 771 ya usalama barabarani, sawa na asilimia 32, ikilinganishwa
na kipindi cha Januari hadi Julai,mwaka jana, ambapo makosa 1,207,832
yalikamatwa.
Kamanda huyo alisema kuongezeka kwa uelewa wa
wananchi juu ya usalama barabarani kwa makundi mbalimbali ya watuamiaji wa
barabara, kumesaidia kupunguza ajali.
Alisema kupungua huko kwa ajali kumetokana na
kushirikiana kwa kupiga simu na kutoa taarifa polisi ili kuwakamata madereva
wanaoshindwa kufuata sheria za barabarani.
Kamanda huyo alisisitiza kuwa, wataendelea kufuta
leseni za madereva watakaobainika kutotii sheria za barabarani bila ya kujali
cheo au umaarufu wa mtu.
No comments:
Post a Comment