WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, imesisitiza udhibiti wa rufaa zisizokuwa za lazima kwa wagonjwa
kutibiwa nje ya nchi, bila kujali wadhifa, cheo au umaarufu wa mtu.
Wataalamu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),
wametakiwa kuhakikisha matibabu yanayowezekana kufanyika katika hospitali hiyo,
yafanywe bila kujali wadhifa wa mtu yeyote.
Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu, alisema hayo
jana, alipozindua vyumba vya upasuaji kwa watoto, ambavyo vimegharimu Dola za
Marekani 675,000 (Sawa na sh. bilioni 1.5) katika Hospitali ya Muhimbili.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara, serikali
inaridhishwa na kasi ya utoaji huduma katika Hospitali ya Muhimbili, ikiwa ni
pamoja na kutekeleza jitihada za serikali ya awamu ya tano ya utoaji wa huduma
bora kwa Watanzania na kupunguza rufaa za kwenda nje ya nchi.
“Ni dhahiri kuwa, ili nia hiyo iweze kutekelezeka,
ni muhimu kuwekeza katika kuboresha miundombinu na kununua vifaa vya kisasa
pamoja na kuwa na wataalamu wa kutosha wenye weledi wa kutoa huduma mbalimbali
za kibingwa,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Waziri Ummy aliwasihi wataalamu kusimamia misingi
ya taaluma zao katika kufanya maamuzi wakati wa kutoa huduma kwa wananchi.
Aliwasihi kuvitunza vifaa vilivyofungwa kwenye
vyumba hivyo vya upasuaji na kuvitumia kwa lengo lililokusudiwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili, Profesa Lawrence Maseru, alisema msaada huo umetoka shirika lisilo
la kiserikali la Archie Wood Foundation la Uingereza.
Alisema vyumba hivyo vitawezesha watoto kufanyiwa
upasuaji mara 10, kwa wiki, badala ya mara tatu kama ilivyokuwa awali.
Alisema hiyo itaondoa kero kwa watoto waliokuwa
wakisubiri kwa muda mrefu kupata huduma hiyo.
Mshauri Mwelekezi wa Upasuaji wa Watoto, Profesa
George Youngson kutoka Archie Wood Foundation, alisema wataendelea kuunga mkono
jitihada za serikali kupitia MHN, katika kutoa huduma za ubingwa wa hali ya juu
ili kupunguza rufaa zisizokuwa za lazima.
Alisema watahakikisha wanatoa msaada wa vifaa tiba,
ikiwezekana kuleta wataalamu nchini
kufanya upasuaji mgumu.
No comments:
Post a Comment