DAKTARI bingwa wa magonjwa ya moyo na tiba kutoka
Hospitali ya Aga Khan, Mustapha Bapumia, ameelezwa kushangazwa na
mfanyabiashara Yussuf Manji kuwa na vyuma kwenye moyo akiwa na umri mdogo.
Amedai kuwa kutokana na hilo, kitaalamu Manji
anatakiwa ajiangalie sana kwa kuwa yupo kwenye hatari na kama anatembea kwenye
kamba nyembamba.
Dk. Bapumia alidai hayo jana, katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha, alipokuwa
akitoa ushahidi kwa upande wa Manji, anayetuhumiwa kutumia dawa za kulevya.
Akiongozwa na Wakili wa Manji, Hajra Mungula, kutoa
ushahidi, Dk. Bapumia alidai alikutana na mshitakiwa huyo, Februari 21, mwaka
huu, ambapo alipelekwa hospitalini hapo akiwa na maumivu ya moyo.
Alidai akiwa na timu yake, walimpokea ambapo tatizo
la moyo kwa Manji ni sugu pamoja na umri wake mdogo.
Shahidi huyo alidai alipata historia ya Manji,
kwamba alizibuliwa mishipa yake ya damu India, Dubai na Marekani na mishipa
mitatu tayari ilikuwa imerekebishwa.
Alidai walimshauri Manji wazibue mshipa, lakini
aliwaeleza waiache kwa sababu familia yake iko Marekani na matibabu yake
hufanyika huko, hivyo aliomba apatiwe dawa.
Shahidi huyo alidai walimwandikia Manji, atumie
dawa nne, ambazo ni za kupunguza koresto, hofu na kama usingizi tatizo na
maumivu sugu ya mgongo.
Alidai Manji aliruhusiwa kutoka hospitalini hapo,
Machi 14, mwaka huu, na siku hiyo hiyo saa mbili usiku, alirudishwa tena
hospitalini hapo, ambapo alilazwa na aliwapa ridhaa wakaingia kurekebisha
chuma.
Alidai kwa wagonjwa wenye matatizo ya moyo, hupewa
dawa zenye morphine kwa ajili ya kupunguza maumivu makali.
Manji
aomba mahakama imuachie huru
Akitoa ushahidi wake, Manji aliiomba mahakama
imuachie huru huku akidai kuwa, dawa anazotumia kutokana na matatizo ya afya
yanayomkabili, zina kiwango kidogo cha morphine na benzodiazephine.
Manji (41), ambaye kwa sasa ni mshauri wa kampuni
za familia, alidai mara ya kwanza aliposomewa mashitaka mahakamani hapo,
alikataa kwa kuamini kwamba angepata nafasi ya kusilizwa ili iweze kutoa uamuzi
wake.
Alidai morphine na benzodiazephine ni sehemu ya
dawa zake, lakini aliona apate nafasi ya kusikilizwa. Manji alidai tuhuma hizo
zimemchafua yeye binafsi na kibiashara.
Manji alidai anatumia dawa za aina tano na kwamba,
amekuwa analetewa uthibitisho na daktari wake kutoka Marekani na mara ya mwisho
kwenda Marekani ni Januari, mwaka huu.
Akielezea historia yake kiafya, Manji alidai ana
matatizo ya moyo, ambayo ni ya kurithi kutoka kwenye familia yake kwani baba na
babu yake walikuwa nayo.
"Nilianza kusumbuliwa tangu nina umri miaka 26
na ripoti zangu zipo tangu mwaka 2002 hadi mwaka jana. Nina vyuma vya kupitisha
damu kwenye moyo, hesabu za daktari vipo vinne za kawaida zimefiki tano,"
alidai.
Alidai kila baada ya miaka miwili, anakwenda
kubadilisha chuma na ripoti za zamani hazijawahi kueleza kama anatumia dawa za
kulevya.
Pia, alidai kwa siku anatumia vidonge 30 hadi 35 na
dawa hizo alipata fursa ya kutumia alipokuwa polisi na hata mahabusu katika
Gereza la Keko.
Kuhusu mashitaka yanayomkabili, Manji alidai
Februari 8, mwaka huu, alipata taarifa kwamba ametajwa kuwa miongoni mwa
watumiaji wa dawa za kulevya na muuzaji, hivyo walitakiwa kuripoti kwa mkuu wa
upelelezi wa makosa ya jinai wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Alidai kwa taratibu za kiofisi, aliitisha mkutano
na vyombo vya habari, ambapo alikana na kueleza hatasubiri kwenda kuripoti
polisi kama alivyotakiwa, bali atakwenda
siku moja kabla.
Manji alidai Februari 8, mwaka huu, alizungumza na
vyombo vya habari na Februari 9, mwaka huu, alienda polisi tangu saa 4.30
asubuhi na katikati ya tarehe hizo alikuwa ofisini.
Alidai morphine inakaa kwenye mkojo ndani ya saa
48. Manji alidai aliamua kwenda polisi
kabla ya tarehe aliyopangiwa kwa sababu hakuwa na taarifa kamili kwani aliipata
kupitia vyombo vya habari na hakutaka kuchafua jina wala kiti chake.
Alidai baada ya kwenda polisi, alipelekwa kwa
mkemia mkuu wa serikali kupima sampuli ya mkojo
na kisha polisi walienda kupekua nyumbani kwale, ambako walichukua
kompyuta yake.
Manji aidai shutuma hizo zimemuathiri binafsi kwa
kuwa wakati yuko mdogo, baba yake alikuwa akimweleza juu ya jina zuri na
maadili kwani zimechafua jina lake.
Pia, alidai anaona aibu kwa watu wanaomfahamu na alianza matibabu mwaka 2009 na amejitahidi
kuacha kuvuta sigara bila mafanikio.
Akihojiwa maswali na Wakili wa Serikali Mkuu, Timon
Vitalis, mshitakiwa huyo alidai daktari
wake hajamkataza kutumia dawa za kulevya kwa ajili ya matibabu.
Alidai amejua morphine ni dawa za kulevya baada ya
kuletwa mahakamani na kwamba, dawa anazotumia anapewa na daktari wake, ambapo
zina uthibitisho na namna ya kutumia.
Shahidi mwingine wa Manji, alikuwa Dk. Khan, ambaye
aliieleza mahakama kumfahamu Manji tangu akiwa na umri wa miaka mitatu, mwaka
1978 na alikuwa akimtibu pamoja na familia yake. Shauri hilo linaendelea leo.
No comments:
Post a Comment