KAMATI ya Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),
inakutana leo, jijini Dar es Salaam, kuanza vikao vyake vya siku mbili, huku
ajenda kubwa ikiwa ni kuwajadili wanachama wake walioomba uongozi katika ngazi
za wilaya.
Kikao hicho kitafuatiwa na kikao cha Halmashauri
Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, ambavyo vyote vitafanyika chini ya Mwenyekiti wa
Chama Taifa, Rais Dk. John Magufuli.
Vikao hivyo ni vya kawaida kwa mujibu wa kanuni na
utaratibu wa CCM, ambapo ajenda kubwa ya vikao hivyo ni kujadili, kupitisha na kufanya uteuzi wa
mwisho wa wagombea wa nafasi za uongozi wa
CCM ngazi ya wilaya.
Kwa mujibu wa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, kamati kuu
inakutana kwa siku mbili, leo na kesho kabla ya kikao cha NEC.
Polepole alisema baada ya vikao hivyo, Septemba 30
na Oktoba mosi, mwaka huu, itakuwa zamu ya vikao vya NEC, ambavyo vitakamilisha
kazi ya uteuzi wa wagombea wa nafasi hizo.
Alisema vikao hivyo vitafanyakazi ya kujadili,
kupitisha na kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea, kabla ya uchaguzi wa CCM
ngazi ya wilaya.
Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi wa CCM na jumuiya
zake, uchaguzi huo kwa wilaya zote umepangwa kufanyika kuanzia Oktoba 2, mwaka
huu, baada ya kukamilika kwa uteuzi wa mwisho.
Vikao hivyo vinafuatiliwa kwa karibu na
wanachama CCM, wakereketwa, mashabiki na
Watanzania kwa ujumla, kutokana mvuto wa ajenda kubwa ya kuwajadili, kupitisha
na kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea wa ngazi za wilaya.
Hatua hiyo inatokana na mkakati wa mabadiliko
unaoendelea ndani ya CCM, wenye lengo la kujenga CCM mpya, itakayokuwa na
viongozi waadilifu na wasio na kashfa za usaliti wala ubadhilifu wa mali za
Chama.
Hivi karibuni, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara,
Philip Mangula, alisema CCM haitamteua mwanachama wake, atakayethibitika kutoa
rushwa na kufanya kampeni kinyume na utaratibu.
Alisema kamati ndogo inaendelea kufuatilia mienendo
ya makada wake, hususan katika maeneo yaliyolalamikiwa na iwapo itathibitika,
hawataeuliwa kugombea uongozi wa Chama.
Tangu kuanza kwa uchaguzi katika ngazi za mashina,
CCM imekuwa ikifuatilia kwa karibu uchaguzi wake, ambapo hivi karibuni,
ililazimika kufuta uchaguzi wa kata zaidi ya 40, kutokana na kasoro mbalimbali
zilizojitokeza kwenye uchaguzi.
Wiki iliyopita, CCM ilikamilisha uchaguzi wa
jumuiya zake katika ngazi za wilaya kwa maana ya UVCCM, UWT na Wazazi, ambapo
baadhi ya viongozi waliochaguliwa ndio watakakuwa wapigakura katika uchaguzi wa
Chama ngazi ya wilaya, unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment