Wednesday, 27 September 2017

IDARA YA UHAMIAJI YATEMA CHECHE KWA WAWEKEZAJI





IDARA ya Uhamiaji nchini, imewataka wawekezaji wote kufuata sheria za nchi, wanapowaajiri wafanyakazi kutoka nje ya nchi.
Imesema wafanyakazi wa viwandani wanaotoka nje, wanatakiwa kufuata taratibu zote, badala ya kuishi na kufanyakazi kinyemela.
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala, aliyasema hayo jana, mjini hapa, alipotembelea shughuli za Kiwanda cha Sukari, Kagera.
Moja kati ya shughuli alizokagua kiwandani hapo ni namna usindikaji wa sukari unavyofanywa katika kiwanda hicho kilichoko wilaya ya Misenyi.
Kamishna Jenerali huyo, pamoja na mambo mengine aliyojifunza, alitumia ziara hiyo kutoa elimu ya uhamiaji kwa watumishi wa kiwanda hicho.
Alisema kuwa na viwanda nchini ni hatua mojawapo ya kujenga uchumi, lakini Uhamiaji ni suala la usalama.
Alisema nchi ikiwa salama, huwavutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza nchini na kufanya shughuli zitakazosaidia kukuza uchumi.
“Wawekezaji wote mliopo hapa nchini, fuateni utaratibu wa sheria za Uhamiaji pale mnapoajiri watumishi kutoka nje ya nchi.
“Watumishi wawe na vibali vya kufanyakazi nchini na vile vya ukaazi, lengo likiwa kuweka nchi salama,”alisema Kamishna Jenerali.
Kwa upande, Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Kagera, Abdallah Towoo, alisema katika kipindi cha mwaka 2016/2017, walikamata wahamiajia haramu 2,426.
Alisema kuwa kati yao, 1,790, walirudishwa katika nchi zao baada ya kukutwa na makosa tofauti.
Vilevile, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu, alisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Alisema moja kati ya changamoto kubwa ni kuwa na mipaka mikubwa iliyo wazi, hali inayowapa wakati mgumu kuwadhibiti wahamiaji haramu wanaoingia nchini kupitia njia zisizo rasmi.
Kwa muda sasa, Idara ya Uhamiaji, imekuwa ikiendesha msako wa wahamiaji haramu na kufanikiwa kuwanasa katika maeneo tofauti.
Hivi karibuni, Uhamiaji iliwakamata wahamiaji haramu wanane, wakiwa kwenye gari inayomilikiwa na mfanyabiashara Aliko Dangote, anayemiliki kiwanda cha kutengeneza saruji kilichoko mkoani Mtwara.
Wahamiaji haramu hao waliokamatwa Mbagala jijini Dar es Salaam, walikuwa wakipelekwa Mtwara.
Mbali ya kudhibiti wahamiaji haramu, Uhamiaji imekuwa ikihakikisha raia wa kigeni wanaofanyakazi nchini, wanakuwa na vibali vya ukaazi.
Kamishna Jenerali yuko mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi ya siku tatu, ambapo atatembelea wilaya za Karagwe, Kyerwa na Ngara.

No comments:

Post a Comment