POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imezionya
kampuni za ulinzi zinazoajiri wafanyakazi katika ulinzi bila kupitia mafunzo ya
JKT na Magambo, kwamba kufanya hivyo ni makosa.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Kamanda wa Polisi
Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alipozungumza na Uhuru,
ofisini kwake.
Alisema kampuni zinazofanya hivyo, zinakiuka
taratibu zinazostahili, kwani zinaajiri baadhi ya watu wasiojua hata namna ya
kushika silaha vizuri.
Kamanda huyo alisema, kutokana na hali hiyo,
wamegundua kuna baadhi ya walinzi wa kampuni binafsi, wanakaa kwenye maeneo yao
ya ulinzi huku silaha wanazotumia wakiwa wameziweka pembeni, jambo ambalo ni
hatari kwa usalama wao na jamii inayowazunguka.
"Ni vyema viongozi au wamiliki wa kampuni hizo,
wakajaribu kuajiri watu waliopita mgambo au JKT ili kuhakikisha wanakuwa na
weledi wa kazi.
“Wanaopitia huko, wanafahamu namna silaha
inavyoshikwa na mbinu zingine za ulinzi," alisisitiza Mambosasa.
Alisema silaha ni kitu muhimu kushikwa na mtu
aliyepewa jukumu la kulinda au aliyeomba kujilinda mwenyewe, badala ya kumpa
mtu mwingine.
Pia, kamanda huyo amewaomba wafanyabiashara kuacha
kubeba fedha nyingi bila kuomba ulinzi wa askari kwa sababu wanahatarisha
maisha yao.
Alikiri kuwepo kwa baadhi ya watumishi wa benki,
ambao siyo waaminifu kutokana na kushirikiana na wahalifu ili kufanikisha
uporaji wa fedha za wateja.
No comments:
Post a Comment