NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Dk. Khamis Kigwangalla, ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU), kuwakamata watu wote waliohusika
kuchakachua sh. milioni 29, fedha za ujenzi wa jengo la Zahanati ya Neruma,
iliyopo wilaya ya Bunda mkoani Mara.
Dk. Kigwangalla, ambaye yuko ziarani mkoani Mara
katika ili kukagua na kuimarisha sekta ya afya, alitoa agizo hilo baada ya kukagua
jengo hilo.
Wakati wa ukaguzi huo, wananchi wakiongozwa na Diwani wa kata ya Neruma, ambaye pia ni Mwenyekiti
wa Halmashauri Wilaya ya Bunda, Isaack Mahela, walimtaka Mkurugenzi wa
Halmashauri kueleza siku maalumu, ambayo jengo hilo litakamilika na kujua
gharama halisi.
“Nakuagiza Mkurugenzi kuhakikisha unawasilisha
nyaraka zote za fedha za jengo hili kwa TAKUKURU na wale wote waliohusika. Wale
waliohusika na uchakachuaji huu, nawakabidhi TAKUKURU wafanye uchunguzi na kuchukua hatua,” alisema naibu
waziri huyo.
Aliongeza kuwa, taifa linataka kusonga mbele, hivyo
watu wanaokwamisha juhudi za Rais Dk. John Magufuli, kuwaletea maendeleo
wananchi, lazima wachukuliwe hatua ili wengine waogope kutafuna fedha za umma.
Jengo hilo, ambalo limeonekana kujengwa chini ya
kiwango, ujenzi wake ulianza mwaka juzi, kwa nguvu za wananchi.
Baadaye, halmashauri ilitenga fedha za kumalizia
mchakato sh. milioni 29, ambazo zimebainika kutafunwa na watendaji waliokuwa
wakishughulikia ujenzi huo.
Dk. Kigwangalla atakuwepo mkoani Mara kwa siku
mbili, ambapo anakagua vituo vya afya, zahanati na hospitali, ikiwa ni sehemu
ya mpango wa uboreshaji sekta ya afya.
No comments:
Post a Comment