Wednesday, 27 September 2017

JPM AITEKA UN


SERIKALI ya Tanzania, imepata heshima kubwa na kuwa kivutio kwenye viunga vya Umoja wa Mataifa, kufuatia utendaji kazi uliotukuka wa Rais Dk. John Magufuli, anayeiongoza serikali ya awamu ya tano.

Heshima hiyo, ilipatikana kwenye mkutano wa 72 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN), unaoendelea jijini New York nchini Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari jana na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Dk. Hassan Abbas, sifa za uongozi wa Rais Magufuli, zimetapakaa katika mkutano huo.

Akizungumza kutoka New York, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga, aliyemwakilisha Rais Magufuli kwenye mkutano huo, alisema Tanzania imekuwa gumzo kutokana na mtindo wa utendaji kazi wa serikali yake, unaolenga kuwakomboa na kuwaletea huduma bora wananchi wake.

“Nimekutana na wajumbe kutoka nchi za Afrika, Asia, Ulaya na wengi wanasema nchi zao ziko tayari Rais Magufuli au viongozi wao wako tayari kuja nchini kupata uzoefu jinsi Rais Magufuli anavyofanya mageuzi makubwa katika kipindi kifupi,” alisema Balozi Mahiga.

Aliongeza: “Nchi hizi zinapishana kutokana na ujumbe wa Tanzania. Mpaka sasa, mbali ya kuhutubia kwenye Baraza Kuu la UN, nimeshafanya mikutano na nchi na taasisi mbalimbali zipatazo 25, wiki hii natarajia kufikisha mikutano 35.”

Waziri Mahiga alitaja kivutio kingine kwa wajumbe wa Tanzania kuwa ni idadi ndogo ya wawakilishi.

Mbali ya Waziri Mahiga, ujumbe huo ulikuwa na maofisa wengine watatu kutoka wizarani kwake, wakiungana na Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Wilson Masilingi.

Akizungumzia ukubwa wa ujumbe aliouongoza, Mahiga alisema hiyo ni historia nyingine, kwani katika mikutano ya UN, Tanzania imekuwa na ujumbe usiopungua watu 40.

Aliongeza kuwa, kuna kipindi ujumbe wa Watanzania, waliwahi kufika idadi ya watu 100, lakini kipindi hiki, maofisa wachache wametekeleza kazi kwa ufanisi.

“Waandishi mbalimbali wa kimataifa walioko hapa, wamekuwa wakifuatilia habari za idadi ya wajumbe na sisi pia walitufuata mpaka tulipofikia. Wameridhika na jinsi Tanzania inavyoenzi matumizi makini ya fedha za walipakodi,” aliongeza Balozi Mahiga.

Pamoja na kutoa salamu maalumu za Rais Magufuli, Balozi Mahiga katika hotuba yake UN, alifafanua mageuzi mbalimbali yanayoendelea nchini, hasa mapambano dhidi ya rushwa na kuimarisha uwajibikaji na akasisitiza utayari wa Tanzania kuendelea kushirikiana na UN.

No comments:

Post a Comment