Wednesday, 27 September 2017

MADIWANI CHADEMA WAWAUMBUA LEMA, NASSARI




MADIWANI wa upinzani waliojiuzulu mkoani Arusha hivi karibuni, wameibuka na kuwashukia wabunge, Joshua Nassari (Arumeru Mashariki) na  Godbless Lema wa Arusha Mjini, kwa kuwaelezea kuwa ni wazushi.

Wamewataka wabunge hao kupeleka ushahidi walionao wa madai ya kununuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ili sheria ifuate mkondo wake.

Madiwani hao walielezea msimamo wao huo jana, baada ya wabunge hao kudai hivi karibuni kuwa, wamenunuliwa ili wajiunge na CCM.

Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Murieti, Credo Kifukwe, alisema jana kwamba, Lema na Nassari ndiyo vinara wa kufanya kampeni za kununua wananchi ili wajiunge CHADEMA.

Kifukwe alisema chama hicho kimejaa ubinafsii kutokana na viongozi wa ngazi za chini kutoshirikishwa kutoa maoni yenye kuleta maendeleo.

“Tunamtaka Lema na Nassari kama wana ushahidi wa sisi kununuliwa, wapeleke TAKUKURU ili ufanyiwe kazi, siyo kulalamika kwenye mitandao ya kijamii,” alisema.

Kifukwe, ambaye aliwahi kuwa Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Arusha Mjini, alisema anafahamu mbinu chafu zinazofanywa na chama hicho kwa ajili ya kuwagombanisha wanachama washindwe kutekeleza majukumu yao.

Alisema alipokuwa katibu wa chama hicho wilaya, alikuwa akiingia kwenye vikao vyote, vikiwemo vya siri vya viongozi wa kitaifa, hivyo anafahamu mipango mingi iliyokuwa ikipangwa kuigonganisha serikali na wananchi.

“Lema na Nassari hawana lolote, nilikuwa naingia kwenye vikao vyote, ninawafahamu vyema na mipango yao yote naijua, wakiendelea kupiga kelele bila kupeleka, nitaweka kila kitu hadharani.

‘’Ninawajua kuliko wanavyofikiri, wakiendelea kutuchafua nitaweka mambo yao wazi mpaka washindwe kutoka ndani na kutembea.

“Mkoa huu sijawahi kukutana na kiongozi yeyote wa CCM wala serikali, atakata kunirubuni ili niache udiwani, nirudi CCM, hizo ni akili zangu.

“Mwizi huamini kuwa kila mtu ni mwizi, ndiyo maana wanafikiri tumenunuliwa, hatujanunuliwa. Nimeamua kurudi CCM kwa hiari yangu ili niweze kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli kutatua kero za wananchi, hasa wanyonge.

‘’Nataka kuwa huru. Kutoka CHADEMA niliamua mwenyewe bila hata kuishirikisha familia yangu. Nataka nimuunge mkono rais na na wateule wake katika mkoa wa Arusha kwa kuchapa kazi.

“Ukiunga mkono juhudi hizi za Rais Magufuli ukiwa CHADEMA, utachukiwa na kuitwa msaliti.
Kwa upande wake, Anderson Sikawa, aliyekuwa Diwani wa Leguruki, alisema siasa wanazofanya Lema na Nassari ni za majitaka na kwamba, hakuna ushahidi wowote walionao.

“Sijanunuliwa na mtu yeyote, hizo ni siasa za majitaka na hakuna mtu anaweza kuninunua. Walinifuata mara kadhaa baada ya kusikia nataka kurudi CCM, wakaniomba nisiondoke, nikagoma nikasema narudi nyumbani.

“Nilikuwa CHADEMA kwa kuamini chama hicho kingetatua kero za wananchi, lakini baada ya Rais Magufuli kuchaguliwa, alianza kupambana na mafisadi, wala rushwa na kutatua kero za wananchi, kwanini nisirudi CCM ili nimuunge mkono?” Alihoji Sikawa.

Mchungaji Japheth Jackson, aliyekuwa diwani wa kata ya Ambureni, alisema taarifa zinazoenezwa na Lema na Nassari, siyo za kweli.

Alisema wabunge hao wameishiwa sera kwani, wameona serikali ya awamu ya tano ikichapa kazi na kuwapelekea wananchi maendeleo, bila kujali itikadi za vyama vyao.

“Wateule wa rais katika wilaya ya Arumeru na mkoa mzima wa Arusha, wanatumikia wananchi kwa moyo wa dhati usiku na mchana, ndiyo walioanza kunihamasisha nimuunge  mkono Rais Magufuli,”alisema.

Kwa mujibu wa Jackosn, kabla ya kufanya uamuzi wa kurudi CCM, alifunga siku 40, akifanya maombi usiku na mchana ili Mungu amsaidie katika uamuzi wake.

Alisema baada ya funga hiyo, Mungu alimpa kibali, akafanya uamuzi wa kuihama CHADEMA.

Alitaja sababu nyingine ya kuondoka kwenye chama hicho kuwa ni kuwepo kwa  mgogoro usiokwisha wa madiwani wenzake, kupinga kila jambo zuri linalofanywa na serikali ya awamu ya tano, ambayo imefanya mambo makubwa.

Akizungumzia kuhusu tuhuma hizo za madiwani, Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Elias Mpanda, alisema kwamba, taarifa hizo ni za uongo na uzushi mtupu.

“Taarifa hizo ni uongo, zimejaa uzushi. CCM ni Chama kikongwe chenye heshima ya pekee ndani na nje ya nchi, kina wanachama zaidi ya milioni nane, wapinzani wanapambana na sisi kwa miaka 25,” alisema.

Alimtaka Nassari kuacha kufanya siasa za maigizo za matukio, akisisitiza kwamba, wanayo dhamana ya kuwatumikia wananchi waliowachagua. 

Kwa mujibu wa Mpanda, licha ya madiwani hao, pia waliwapokea wanachama wengine 480, kutoka vyama mbalimbali vya upinzani waliohamia CCM.

“Lema mwenyewe kabla ya kuhamia CHADEMA, alikuwa TLP, atuambie alinunuliwa kwa shilingi ngapi?” Alihoji.

Alisema wanasiasa hao wamekosa sera na kwamba, wananchi wamekuwa na imani kubwa kwa CCM, hususan katika kipindi cha uongozi wa serikali ya awamu ya tano, chini ya Dk. Magufuli, inayohangaika na shida za wananchi wanyonge.

No comments:

Post a Comment