ALIYEKUWA Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar),
Nassor Seif Amour, amesema upande unaomtii Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa
Ibrahim Lipumba, hauko tayari kufanya mazungumzo ya upatanishi na Katibu Mkuu
aliyesimamishwa kazi, Maalim Seif Sharrif Hamad.
Amesema muda wa kumshirikisha Maalim Seif katika harakati
za kisiasa visiwani Zanzibar, umepita na mwanasiasa huyo amejiondolea heshima
na amana ya kisiasa katika jamii.
Akizungumza na Uhuru, nyumbani kwake Michenzani, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, Nassor alisema, CUF upande unaoheshimu katiba, umefunga milango ya upatanishi na kiongozi huyo.
Kwa mujibu wa Amour, kuanzia sasa mbunge yeyote ambaye atakaidi matakwa ya kikatiba ya chama, kukataa kushiriki vikao vya kikatiba, kukaidi au kupuuza mamlaka ya mwenyekiti, atafukuzwa uanachama mara moja.
"Tumekubaliana kufunga milango ya upatanishi na Maalim Seif ndani ya CUF ili kumpa nafasi ajiunge na CHADEMA. Amepoteza imani kwa wananchi, hivyo kukubali kumrudisha ndani ya chama ni kujivika kitanzi cha kisiasa,"alisema.
Mwanasiasa huyo, ambaye kwa sasa ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Oganaizesheni Taifa, alisema kitendo chake cha kuwatangazia wananchi kuwa ataapishwa kuwa Rais mpya wa Zanzibar, wakati alisusia uchaguzi wa marudio, kimewakera wanachama na mashabiki wa chama hicho.
Alieleza kuwa, msimamo wa chama chao kwa wakati huu ni kuendelea na maandalizi ya kushiriki uchaguzi ujao mwaka 2020 na kusahau kabisa jina la Maalim Seif kuwania urais kupitia CUF.
"Tunajua na tuna habari za uhakika mwaka 2020, atasimama kuwania urais kwa tiketi ya CHADEMA. Sisi tumenawa mikono yetu. Tunamruhusu na kumtakia maisha mengine mapya ya kisiasa kwenye chama kipya,"alisisitiza
Huku akimshutumu Maalim Seif, Nasor alisema, shughuli za ujenzi wa chama hicho, zinaendelea kama kawaida chini ya Kaimu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya.
Alisema Maalim Seif na wenzake, siku watakapotangaza rasmi kuhamia CHADEMA, watalazimila kuliacha jengo la makao makuu ya chama hicho, lililoko Mtendeni, mjini Unguja ili kusaka makazi mapya.
"Ofisi ya Mtendeni ni makao makuu ya CUF kwa mujibu wa katiba na utaratibu wa usajili. Tungependa kuona watakapohamia CHADEMA, waliache jengo la chama chetu mikononi mwetu au tutawashitaki mahakamani,"alieleza.
Nassor, ambaye ni miongoni mwa waasisi wa CUF mwaka 1992, alisema chama chao kitaendelea kuheshimu kanuni na katiba yake chini ya Mwenyekiti Profesa Lipumba na kusimamia sheria za nchi na kujenga hoja za kikatiba hadi uasi utakapokoma.
"Tumekuwa tukitetea haki za Wazanzibari na kupigania mageuzi ya demokrasia kabla na baada ya usajili wa CUF kisheria. Tumepingana na viongozi mafisadi, wezi na waliochukua mali za umma. Ni ajabu kumuona Maalim Seif na wale aliowatuhumu, akiwafanya marafiki na wenzake akiwageuza maadui,"alisema.
Alipotafutwa kwa njia ya simu ili kujibu tuhuma hizo, Maalim Seif hakuweza kupatikana kwa njia simu kwani muda wote ilikuwa ikiita bila kujibiwa.
Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno, hakuonyesha ushirikiano wowote hadi wakati tukienda mitamboni.
No comments:
Post a Comment