WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba,
amesema uchunguzi unaofanywa baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi
Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu, umebaini mambo mazito,
hivyo Watanzania wavute subira.
Aidha, Mwigulu amesema gari aliyoitaja Lissu,
ilifuatiliwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Nchini
(DCI), ikabainika kwamba, iko Arusha na haikusafiri kuelekea alikokuwa mbunge huyo.
Pia, amesema aliyemtolea bastola Mbunge wa Jimbo la
Mtama, Nape Nnauye, siyo askari polisi kwa sababu hakuvaa sare, hivyo ni vigumu
kumbaini.
Mwigulu alitoa kauli hiyo jana, alipohojiwa kwenye
kipindi cha 360, kinachorushwa na kituo cha Televisheni cha Clouds, kilichopo
jijini Dar es Salaam.
“Tunamuombea Lissu apone, nina imani akishapona,
atatupa mchango mkubwa wa kusaidia uchunguzi. Mnajua mtu akiwa kwenye maumivu
makali, huwezi kumuuliza lolote,” alisema.
Mwigulu alisema, kutokana na upya wa uhalifu wa
aina iliyotokea kwa Lissu, kuna mambo wanaendelea kuyafuatilia, ambayo hawezi
kuyaeleza hadharani mpaka uchunguzi ukamilike.
“Suala la Lissu kutokana na upya wake, kuna vitu
tunaendelea kuvifuatilia, hivyo kuna mambo hatuwezi kuyasema sasa,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka Watanzania
kuendelea kuwa na subira kwa sababu kazi inaendelea kufanyika.
Mwigulu alisema baada ya tukio la kushambuliwa
Lissu, Septemba 7, mwaka huu, taarifa kadhaa zilichukuliwa eneo la tukio,
ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi ili kupata undani wake.
“Wahalifu hawajakamatwa wote, ukianza kusema
itakuwa ni shida, kuna mambo yanaendelea kufanywa na hayana ukomo.
“Ukomo utafikiwa endapo wote waliohusika
watakamatwa. Nikisema naweza kuvuruga kazi inayoendelea,” alisema.
Hata hivyo, alipoulizwa watu wanahoji kwamba,
askari wanapouawa, wahalifu wanakamatwa mapema, kuna tofauti gani na hili?
Alijibu: " Watu wakiwaza hivyo, watakuwa wanakosea,
hatuweki madaraja, ni mazingira ya tukio tu.”
Akizungumzia uchunguzi unaoendelea kuhusu kuvamiwa
kwa Lissu, alisema hawezi kueleza waliokamatwa, lakini tayari kuna magari zaidi
ya 10, yanayofanana na lililohusika kwenye tukio yamekamatwa.
Kuhusu kumtembelea Lissu hospitalini, alisema
alimuona siku ya tukio Septemba 7, mwaka huu, akiwa katika Hospitali ya Rufaa
Dodoma, baadae uwanja wa ndege, aliposafirishwa kwa ajili ya matibabu jijini
Nairobi, nchini Kenya, ambako yuko hivi sasa.
"Sijafika Nairobi kumjulia hali Lissu, bali
kwa mkoa wa Singida, Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu amefika.
“Katika mazingira mengine, tunaendelea kupata
taarifa, kama serikali tunaye balozi,
kama waziri kwenda kumuona ni jambo jema katika utaratibu wa uchunguzi,
hata dereva tutazungumza naye,” alisema.
Septemba 7, mwaka huu, Lissu alishambuliwa na
kujeruhiwa kwa risasi na watu wasiojulikana, alipokuwa akielekea nyumbani kwake
Dodoma.
No comments:
Post a Comment