Monday, 14 September 2015

DIANA CHILOLO AMLIPUA TUNDU LISSU



NA JUMBE ISMAILLY, IKUNGI     

MJUMBE wa Halmashauri Kuu Taifa (CCM), Diana Chilolo, amewatahadharisha wananchi wa jimbo la Singida Mashariki, kutomchagua mgombea wa CHADEMA, Tundu Lissu, kutokana na kutokujenga nyumba kwao.

Diana, ambaye ni Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Singida, alisema hayo kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza kwenye mikutano ya hadhara ya kampeni za kumnadi mgombea wa ubunge wa jimbo hilo, Jonathan Njau, iliyofanyika jana kwenye kata ya Mang’onyi, tarafa ya Ikungi.

Alisema Lissu pamoja na kukaa Bungeni kwa kipindi cha miaka mitano na kupokea mshahara na posho mbalimbali za Bunge,ameshindwa kujenga nyumba ya kuishi yeye na familia yake akiwa jimboni.

“Niwaambieni kitu kingine, Tundu Lissu pamoja na kukaa bungeni miaka yote mitano,mimi mwenyewe mwanamke hapa nina nyumba yangu Singida mjini na bado nina nyumba nyingine kule nilipozaliwa Shelui,lakini Tundu Lisu hana nyumba kwao Mahambe, hana nyumba hapa,”alisema.

Kwa mujibu wa Diana, Lissu anapotoka Dodoma au kwenda Dar es Salaam , huwa anafikia kwenye nyumba ya kulala  wageni.

“Hivi kweli kiongozi anayefikia kwenye nyumba ya kulala wageni sisi wazee, sisi kina mama tumfuate ‘guest' ? Wewe mke wa mtu umfuate mbunge  huko, ukizuliwa la kuzuliwa, si matatizo hayo jamani?" Alihoji.

Aliwataka wananchi wa jimbo hilo kumchagua kiongozi atakayejali nyumbani kwao na hata anapotafutwa inakuwa rahisi kumpata.

Aliweka bayana kuwa Lissu haoni sababu ya wananchi wake kuwa na kituo cha kutolea huduma za afya, hususani kina mama wajawazito kwa kuwa mke wake anapokuwa na mimba, humpeleka kujifungulia Marekani.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa jimbo hilo, Njau  aliwaomba wananchi wamchague kuwa mbunge wa jimbo hilo
huku akisisitiza kuwa katika kipindi chake cha uongozi wake, atawashughulikia watendaji wanaokula fedha za umma.

No comments:

Post a Comment