Monday, 14 September 2015

CCM YAIBOMOA CUF LINDI

HABARI ZOTE NA ABDALLAH MWERI, LINDI

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeibomoa ngome ya CUF mkoa wa Lindi, baada ya wanachama wake kurudisha kadi kwa madai ya kuchoshwa na mwenendo mbovu wa uongozi wa juu.

Tukio hilo lilitokea juzi jioni kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea mwenza wa urais kupitia CCM, Samia Suluhu Hassan, uliofanyika kwenye Uwanja wa Mnazi Mmoja, Jimbo la Lindi Mjini.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa NEC ya CCM, Nape Nnauye, aliongoza mapokezi ya wanachama hao waliodai kuwa wamerejea nyumbani kutokana na kukerwa na ubabaishaji wa viongozi wa CUF.

Viongozi wengine waliopanda jukwaani kupokea kadi za wanachama hao ni Mke wa Rais Mama Salma Kikwete, aliyewataka wakazi wa Lindi Mjini kuipigia kura za kishindo CCM.

Salma alisema wakazi wa Lindi Mjini wanatakiwa kufanya uamuzi sahihi wa kumchagua mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli ili kumpata Samia, ambaye atakuwa makamu wa kwanza wa rais mwanamke katika historia ya Tanzania.

Mmoja wa wanachama wa CUF, Bakari Kalulu, alisema chama hicho kimepoteza dira baada ya kujiunga na UKAWA na uongozi kukubali kumpokea mgombea wa urais wa CHADEMA, Edward Lowassa.

Kalulu alisema baada ya kufanya kazi nzuri ya kuimarisha CUF, wamejiunga na CCM, ambapo waliahidi kumpigia debe mgombea wa Chama, Dk. John Magufuli, katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

"Wanachama tunaoihama CUF tuko wengi hapa Lindi Mjini, sisi ni wachache, tumeamua kupanda jukwaani kuwakilisha wengine, tumejiunga na CCM baada ya kuchoshwa na uongozi mbovu akiwemo mbunge Baruan," alisema Kalulu.

Naye Abdallah Madebe, alisema amerejea CCM kuimarisha chama katika mkoa wa Lindi, ambako CUF imekuwa na nguvu kubwa. Mbunge wa Lindi Mjini ni Salum Baruan kutoka CUF.

Madebe aliwataka radhi wakazi wa Lindi Mjini kwa kushiriki kumuweka katika uongozi Baruan, ambapo alidai katika kipindi cha miaka mitano hakuwapa maendeleo wananchi wa jimbo hilo.

"Katika mambo ambayo nitajutia ni kushiriki usiku na mchana kumsaidia Baruan kupata ubunge. Najuta kwa sababu katika muda wote wa miaka mitano, hakuna alilofanya zaidi ya kututia unyonge wakazi wa Lindi Mjini," alisema Madebe.

Madebe alimtaka Nape na viongozi wa CCM kutokuwa na hofu ya kulikomboa Jimbo la Lindi Mjini kutoka CUF, kwa sababu wanajua mbinu za ushindi na wanachama wengi wanatarajia kukihama chama hicho.

Alisema CUF imerudisha nyuma maendeleo ya wakazi wa Jimbo la Lindi Mjini, ambao wanakosa huduma muhimu zikiwemo maji, vituo vya afya, zahanati na elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Kwa upande wake, Samia alisema hatua ya wanachama wengi kutoka Lindi Mjini kujiunga na CCM, inadhihirisha chama hicho kinavyotekeleza kikamilifu Ilani ya Uchaguzi.

"Jamani wenyewe mmeona tena hawa ni wachache tu, wako wengi sana wameshindwa kupanda jukwaani, CCM ni chama bora mfano wa kuigwa, tunawakaribisha sana karibuni nyumbani," alisema Samia.

Mgombea mwenza huyo aliwataka wakazi wa Jimbo la Lindi Mjini kumchagua Hassan Kaunja, anayewania ubunge kwa tiketi ya CCM, madiwani na mgombea urais, Dk. John Magufuli.

No comments:

Post a Comment