Monday, 14 September 2015

SAMIA: WEKEZENI KATIKA ELIMU


MGOMBEA mwenza wa urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM),  Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi wa mkoa wa Lindi kuwekeza katika elimu.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni, Samia alisema rekodi zinaonyesha kuwa wananchi wa mkoa wa Lindi hawana mwamko wa kusoma, hatua ambayo inahatarisha ustawi wa maisha yao kiuchumi.

Samia, alitoa kauli hiyo kwa wakazi wa Jimbo la Lindi Mjini, ambako alifanya mkutano wa kampeni katika uwanja wa Mnazi Mmoja.

Alisema serikali ya awamu ya tano imejipanga kikamilifu kutekeleza Ilani ya Uchaguzi katika sekta ya elimu na mkoa wa Lindi ni miongoni mwa mikoa michache inayotakiwa kuongeza kasi.

"Jamani naomba sana wakazi wa Lindi muwekeze katika elimu, serikali ya awamu ya tano imejipanga vizuri kutekeleza ilani ya uchaguzi, lakini lazima na nyinyi wenyewe mjitahidi. Haitakuwa na maana tukajenga mabweni na madarasa halafu hakuna wanafunzi," alisema Samia.

Alisema haitakuwa na maana endapo serikali itajenga majengo mazuri ya shule za msingi na sekondari, lakini wanafunzi wenye mwamko wa kusoma ni wachache ikilinganishwa na idadi ya wavulana na wasichana walioko mkoani hapa.

Samia, aliwataka wananchi wa Lindi kuhimiza watoto wao kupata elimu kwa sababu Mungu ameagiza katika vitabu vyake kuwa elimu ni jambo la msingi kwa binadamu.

"Nimesikia kilio cha mbunge wenu kuhusu ujenzi wa shule ya sekondari ya kidato cha tano na sita, hakuna tatizo serikali ya awamu ya tano itatekeleza, lakini sio shule inajengwa halafu darasani wanaingia wanafunzi wanane, haitaleta maana," alisema Samia.

Mgombea mwenza huyo aliwataka wakazi wa Lindi Mjini kumchagua Dk. Jonh Magufuli kuwa rais wa awamu ya tano kwa kuwa ataleta maendeleo ya wananchi ikilinganishwa na UKAWA.

Alisema baadhi ya vipaumbele katika serikali ya Dk. Magufuli ni kuongeza ajira kwa vijana, kuboresha huduma za afya na elimu katika kila kata nchini.

Wakati huo huo, Samia amewataka wakazi wa Lindi Mjini kumchagua, Hassan Kaunje kuwa mbunge pamoja na madiwani wa CCM ili kuharakisha maendeleo ya jimbo hilo.

No comments:

Post a Comment