Monday, 14 September 2015
NAPE AMTAKA BARUAN AJITOE KUWANIA UBUNGE
KATIBU wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, amemtaka mbunge wa Jimbo la Lindi Mjini kupitia CUF, Salum Baruan, kujiondoa katika mbio za kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza na wakazi wa Mnazi Mmoja, Lindi Mjini, Nape alisema CCM italikomboa jimbo hilo katika uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Alisema Baruan amepoteza mvuto kwa wakazi wa Lindi Mjini, baada ya kushindwa kuwatumikia katika kipindi chote cha miaka mitano iliyopita tangu alipochaguliwa kuwa mbunge katika uchaguzi mkuu mwaka 2010.
"Kama ana akili, marupurupu aliyopata bungeni ni vizuri akatumia pesa hizo na mkewe nyumbani kwa sababu atapata aibu ya mwaka," alisema Nape.
Katibu huyo wa NEC alisema CCM imejipanga kikamilifu kuhakikisha Jimbo la Lindi Mjini linarejea katika mikono ya CCM na CUF haina ubavu wa kushinda, baada ya Baruan kuwahadaa wananchi kwa miaka mitano bila kuwaletea maendeleo.
Nape alisema Lindi Mjini inayo mitaa 117 na CCM imeweka katika himaya yake mitaa 85, ambayo ina uhakika itashinda kwa kishindo kwa kumchagua Hassan Kaunje kuwa mbunge.
Mgombea mwenza wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, amesema endapo watamchagua Kaunje kuwa mbunge wao, jimbo hilo litapata maendeleo haraka katika serikali ya awamu ya tano.
Alisema wakazi wa Lindi Mjini wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu kwa kuwa mbunge wao hakuwa mstari wa mbele kuwaletea maendeleo, hivyo Oktoba 25, mwaka huu, wasifanye kosa kumrejesha bungeni.
Samia alisema serikali ya awamu ya tano itakuwa karibu na Kaunje kushughulikia kero za wakazi wa Lindi Mjini, zikiwemo maji safi na salama, vituo vya afya na kupandisha kiwango cha elimu.
"Serikali ya awamu ya nne imejipanga vizuri kutekeleza Ilani ya Uchaguzi, kero zenu zote zimo katika ilani, nimesikia kilio chenu wakati nanong'ona na viongozi wenu, nimezichukua changamoto zenu tutazifanyia kazi," alisema Samia.
Samia, ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), aliwataka wakazi wa Lindi Mjini kumchagua Dk. John Magufuli kuwa rais wa awamu ya tano.
Ziara ya mgombea mwenza huyo inaendelea katika mikoa ya Lindi na Mtwara. Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani umepangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment