NA MWANDISHI WETU, PEMBA
WAKATI CCM ikitarajia kuzindua kwa kishindo kampeni zake kwa upande wa kisiwa cha Pemba, CUF imeambiwa haina hati miliki na majimbo ya kisiwa hicho.
Imetakiwa kuacha vitisho na kujiandaa matokeo ya kushitusha pale itakapopoteza majimbo hayo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, 25 mwaka huu.
Aidha, CCM imeweka mkakati mzito kuhakikisha inawaunga mkono wananchi wa Pemba waliopanga kukitosa chama hicho baada kushindwa kutimiza ahadi zake licha ya kuaminiwa zaida ya mara nne kwenye uchaguzi mkuu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd amesema Serikali ya CCM kamwe haitasita wala kuchelea kupeleka nyenzo za maendeleo katika kisiwa cha Pemba kwa sababu ya kukosa majimbo ya uwakilishi na ubunge tangu mwaka 1995.
Balozi Seif alitoa msimamo huo wakati akihutubia mkutano wa hadhara ulofanyika katika Kijiji cha Michakweni Shehia ya Kiwani Mkoa wa Kusini Pemba.
Alisema maendeleo yanayooneka sasa kisiwani humo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, vituo vya afya, madarasa, miradi ya maji na kupelekwa nishati ya umeme wa grid ya Taifa ni utekelezaji wa sera za CCM na serikali yake.
"Wakati umefika kwa wananchi wa Pemba kuamua na kufanya mabadiliko ya kihistoria, wapeni talaka na kuwaweka benchi wabunge na wawakilishi kupitia CUF, hawana jipya na wameshindwa kazi mliyowatuma," alisema.
Aidha, aliwahakikishia wananchi wa Pemba kwamba mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad hatashinda uchaguzi wowote Zanzibar kwa sababu hatoshi na amepungukiwa sifa ya kuaminiwa kuwa urais wa nchi.
Alisema mgombea huyo ataingia katika orodha ya kitabu mashuhuri cha guiness, kwa kua kiongozi aliyeshiriki uchaguzi mara nyingi kuliko mwanasiasa yeyote katika Afrika Mashariki na kati huku mara zote akianguka vibaya.
"Alichuana na Mzee Idris Abdul Wakil wakati wa chama kimoja akapigwa mwereka, akapambana na Dk. Salmin Amour mwaka 1995 akashindwa, akashindana na Dk. Amani Karume akaangukia pua, alipojipima ubavu na Dk. Shein pia akabwagwa vibaya. Mwaka huu pia ataachwa solemba," alisema.
Alisema CUF imepoteza sifa ya kuwa chama cha kidemokrasia kutokana na kumsimamisha mgombea mmoja wa kudumu kana kwamba chama hicho hakina wanachama wengine.
Pia alisema ni jambo la kusikitisha sana kuona makamu Mwenyekiti wake Juma Duni Haji akiiuzwa kwa mkopo katika chama cha Chadema kwa ajili ya tamaa ya kusaka madaraka.
SHAKA: CCM HAIBAHATISHI
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alisema CCM haibahatishi katika kuendesha utawala wa dola bali ina malengo na dhamira ya kulinda na kusimamia usalama, uhai na maisha ya wananachi wote bila ubaguzi.
Shaka alisema CUF haina hatimiliki ya kushinda uchazguzi kwenye majimbo ya Pemba na kwamba mwaka huu ni zamu ya CCM kuyarudisha majimbo hayo.
Shaka alisema CUF wamejisafishia njia ya kushindwa kutokana na ubinafsi na ubabaishaji inaoufanya kwenye kuwatumikia wananchi wa Pemba.
"Tunawatumia salamu na kesho (leo) zitawafikia wakati tutakapozindua kampeni kwa upande wa Pemba.
"Wameshawadanganya sana wananchi wa pemba hivi sasa inapaswa kuwa mwisho majimbo yote ya Pemba tunayataka na kwa jinsi Maalim Seif na CUF walivyoshindwa kuonyesha mfano katika kuwaletea maendeleo, tunaamini tutashinda uchaguzi wa mwaka huu mapema," alisema.
Kwa mujibu wa Shaka ushindi wa CCM mwaka huu hauna mjadala kwa kuwa imefanya maandalizi makubwa ikiwa ni pamoja na kuwatumikia wananchi na kutekeleza ahadi zake ilizotoa kupitia Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2010-2015.
MKE WA BALOZI IDDI AOMBA KURA
Naye Mke wa Makamau wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mama Asha Suleiman Idd, alisema ushindi wa CCM hauwezi kupatikana bila ya kura za Pemba na kwamba uchaguzi wa Oktoba, mwaka huu, ni wa kufa na kupona.
Mama Asha aliwataka wananchi wa Kiwani kufanya uamuzi wa kihistoria ili kuachana na ahadi hewa zinazotolewa na viongozi wa CUF ambazo tangu kuingia mfumo wa vyama vingi zimekuwa hazitimii hivyo kutopatikana kwa matunda yake.
"Waswahili wa zamani wamesema akili za kuambiwa changanya na zako, ahadi nyingi zimetolewa na Maalim Seif ambazo hadi sasa ziko hewani, pitisheni uamuzi wa kukikataa chama hicho na kufungua ukurasa mpya kwa maendeleo yenu," alisema.
Alisema CCM iliyotokana na TANU na ASP vyama ambayo kwa makusudi vilipigania uhuru na mapinduzi ya Zanzibar ili kuwapa hadhi, heshima, kutambuliwa utu wa kila mmoja, mmejaribu kuwachagua wawakilishi na wabunge wa CUF kwa miaka 20 bila mafanikio, badilini upepo na kuchagua CCM," aliwaomba wapiga kura wa Pemba.
No comments:
Post a Comment