Friday 13 October 2017

UTOROSHAJI MADINI SASA BASI- ANGELLA


WAZIRI wa Madini, Angellah Kairuki, ametaja vipaumbele vyake katika wizara hiyo kuwa, ni pamoja na udhibiti wa utoroshaji wa madini na kupigania maslahi ya wafanyakazi.

Amewataka watumishi wa wizara hiyo na idara zilizo chini yake, kufanyakazi kwa uadilifu na weledi wa hali ya juu.

Kairuki aliyasema hayo jana, jijini Dar es Salaam, alipozungumza na  watumishi wa wizara hiyo na taasisi zake, makao makuu ya wizara hiyo walioko Dar es Salaam na Makao Makuu, Dodoma.

Alisema sekta ya madini inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi na kuwataka wataalamu wa madini, kubuni mbinu za ukusanyaji maduhuli na kuboresha mazingira ya uwekezaji kwenye uchimbaji madini.

Aidha, aliwataka wataalamu hao kubuni mikakati ya kuzuia utoroshaji wa madini nchini ili nchi ipate mapato stahili.

Amewataka watumishi kuepuka kufanyakazi kwa mazoea, badala yake wawe
wabunifu ili sekta hiyo iwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Kwa upande wake, Naibu  Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, aliwakumbusha watumishi hao kuzingatia dira na dhima ya wizara, ikiwemo kufanyakazi kwa tija ili hatimaye sekta ya madini iweze kuchangia katika uchumi wa taifa.

Lengo la kikao hicho lilikuwa kujitambulisha, kufahamiana na kupanga mikakati ya kushirikiana ili kuhakikisha sekta ya madini inakuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Taasisi zilizoshiriki kikao hicho ni Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Chuo cha Madini Dodoma (MRI), Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini na Mpango wa Kuongeza Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji (TEITI).

No comments:

Post a Comment