Friday, 13 October 2017
DK. SHEIN AKEMEA UUZAJI ARDHI HOLELA
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema wananchi wanaouza ardhi na wengine kukata viwanja kwa ajili ya kujenga nyumba za kuuza, wanaharibu mpango wa serikali wa kutoa eka tatu kwa ajili ya kilimo.
Amesema serikali katika awamu zote, imekuwa na mpango huo kwa ajili ya kuimarisha kilimo na kuongeza tija katika uchumi.
Dk. Shein aliyasema hayo jana, katika ufunguzi wa maonyesho ya Siku ya Chakula Duniani, yaliofanyika Kizimbani na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd, Mama Mwanamwema Shein na viongozi wengine wa vyama vya siasa na serikali.
Rais Dk. Shein alisema kitendo hicho siyo kizuri kwani kinavunja mwelekeo na azma ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 na kusababisha vizazi vijavyo kukosa sehemu za kilimo, jambo litakalowalazimu kuagiza chakula nje ya nchi.
Aliongeza kuwa, ipo haja ya kuzingatia matumizi mazuri ya ardhi ndogo iliyopo kwa kutenga maeneo ya kilimo, makazi na shughuli nyingine za kiuchumi kwa kuzingatia sheria za mipango miji na vijiji.
Kwa mujibu wa Dk. Shein, hivi sasa Zanzibar ina watu milioni 1.4, hali inayochangia kuwa na matumizi makubwa ya ardhi, hususan makazi na kupunguza ardhi ya kilimo.
Aliwataka wananchi wanapotaka kujenga, ni vyema wapeleke maombi yao Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira ili waelekezwe utaratibu uliopo.
Dk. Shein alisema, hivi sasa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeamua kufanya mapinduzi ya kilimo kwa kuingia kwenye kilimo cha kisasa na cha kitaalamu, hatua ambayo imeanza kuzaa matunda kwa kuongezeka mavuno ya mazao mbalimbali, hususan chakula.
Alieleza kuwa, mavuno ya mpunga yaliongezeka kutoka wastani wa tani 33,655.06, mwaka 2013 hadi tani 39,000, zilizovunwa mwaka huu, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa kwa miaka 10 iliyopita.
Dk. Shein alisema kwa upande wa mazao ya matunda, mavuno yaliongezeka kutoka wastani wa tani 15,000, mwaka 2015/2016 hadi tani 27,000, mwaka 2016/2017.
"Mafanikio haya yalitokana na matumizi ya mbinu za kilimo cha kisasa na kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa kilimo,"alisema.
Dk. Shein alieleza kuwa, serikali inazingatia umuhimu wa kilimo cha umwagiliaji, hususan kwa zao la mpunga, ambapo kwa kushirikiana na Benki ya Exim ya Korea, itatumia wastani wa Dola za Marekani milioni 50, kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji wa hekta 1,524.
Alisisitiza kuwa, lengo la serikali ni kuongeza mavuno ya mpunga nchini, kupunguza na hatimaye kuondoa kabisa utegemezi wa mchele kutoka nje ya nchi, ambapo hivi sasa kwa kila mwezi, Zanzibar inaingiza wastani wa tani 7,259 za mchele.
Kwa upande wa zana za kilimo, Dk. Shein alisema katika kuziendeleza na kuimarisha huduma za matreka, serikali imeandaa mpango madhubuti wa Kiwanda cha Matrekta cha Mbweni kuwa wakala kwa mujibu wa sheria na kukipa hadhi yake inayostahili katika kilimo.
Alisema walikubaliana na Kampuni ya Mahindra ya India, kwa lengo la kuleta matrekta mapya 100, zana nyingine za kilimo na hivi karibuni, serikali ilitia saini kuletewa matrekta 20, ambapo kwa kuanzia, yameshapokelewa 10 yakiwa yanatoka Libya.
Awali, Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Hamad Rashid Mohamed alisema maonyesho hayo ni katika kutekeleza maagizo ya Dk. Shein,kutayarisha maonyesho hayo yanayoendana na sikukuu ya wakulima ya nanenane, huku akieleza haja ya kuwepo kiwanja kama hicho kisiwani Pemba, kwa madhumuni kama hayo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Joseph Abdalla Meza, alisema eneo hilo limetengwa kuwa la kudumu, lenye heka 16, ambapo miongoni mwa shughuli zilizofanyika ni kuweka uzio, njia, miundombinu ya maji, umeme kwa gharama ya sh. milioni 89. Alisema hadi kukamilika kwa majengo ya kudumu, gharama zitakuwa sh. milioni 223.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment