Friday, 6 October 2017

JPM: SERIKALI IMEDHAMIRIA KUTAFUTA MAFUTA




RAIS Dk. John Magufuli, amesema serikali ya awamu ya tano, imedhamiria kufanikisha utafutaji na upatikanaji wa mafuta yaliyopo katika Bonde la Eyasi Wembere ili Tanzania ianze kunufaika na rasilimali hiyo.
Dk. Magufuli, aliyasema hayo jana, muda mfupi baada kupokea taarifa ya maendeleo ya utafiti wa mafuta katika maeneo ya Bonde la Ufa la Eyasi Wembere, Wilaya ya Tanganyika, mkoani Rukwa, iliyowasilishwa na timu ya wataalamu wa Tanzania na Uganda.
Timu hiyo imeelezea uwepo wa viashiria vya uhakika vya kijiolojia,  vinavyothibitisha kuwepo kwa mafuta katika maeneo ya Senkenke, Mwanzugina Kining’inila katika Bonde la Manonga, Wilaya ya Igunga, Mkoani Tabora.
Katika mkutano huo, uliohudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani na Balozi wa Uganda nchini, Richard Kabonero, timu ya wataalamu hao, ilisema miamba, uoto na uwepo wa Bonde Eyasi Wembere katika mfumo mmoja wa bonde la Afrika Mashariki, unaofanana na maeneo mengine yaliyothibitika kuwa na mafuta, ni kiashiria muhimu cha kuwepo mafuta.
Kutokana na taarifa hiyo, Rais Magufuli alisema, serikali ya awamu ya tano ipo tayari kutekeleza shughuli zote zitakazowezesha kupatikana kwa mafuta katika Bonde la Eyasi Wembere na amewaagiza wataalamu wa Tanzania, kuendelea kufanyakazi kwa ukaribu na wataalamu wa Uganda, ambao wana uzoefu wa kupata mafuta katika Ziwa Albert nchini humo.
Rais Magufuli aliwashukuru wataalamu wa Uganda, wanaoshirikiana na wale wa hapa nchini, katika kazi hiyo na amemuomba Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini wa Uganda, Robert Kasandeku, amfikishie shukrani zake kwa Rais Yoweri Museveni kwa ushirikiano anaoutoa.

No comments:

Post a Comment