SAKATA la vifo vya watu 10, waliopoteza maisha kwa
kunywa pombe haramu ya gongo, limefikishwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa
ajili ya uchunguzi zaidi.
Hatua hiyo imefikiwa kwa ajili ya kubaini aina ya
sumu iliyokuwepo kwenye pombe hiyo.
Oktoba 04, mwaka huu, watu 10 walifariki dunia kwa
kunywa pombe haramu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, jana, Kamanda wa
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema jana kuwa, ili kubaini aina ya sumu iliyokuwa kwenye pombe
hiyo, wamelazimika kupeleka vielelezo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.
Mambosasa alivitaja vielelezo hivyo kuwa ni chupa
tatu zenye ujazo wa lita moja, zilizokuwa na kinywaji hicho haramu, ambazo
ziliokotwa eneo la Kimara Stop Over.
"Tulivipata vielelezo hivyo katika pagala
lililokuwa likitumika kwa ajili ya uuzaji wa pombe hiyo haramu, tumevipeleka
kwa mkemia kwa uchunguzi zaidi,” alisema Mambosasa.
Aliongeza: “Inasikitisha na kushangaza kuona eneo hilo likitumika kwa shughuli ya
kuuza pombe haramu, kwani hapo ni eneo lililovunjwa, ambako muuzaji huyo
anaendelea na biashara haramu."
Alisema wamegundua ‘pagala’ hilo kufuatia upelelezi
wa kina uliofanywa na polisi, kwamba lilibaki baada ya bomoa bomoa kwa baadhi
ya nyumba kufanyika.
Alisema muuza gongo huyo ajulikanae kwa jina moja
la Hanoza, ni miongoni mwa waliofariki kwa kunywa kinywaji hicho.
Mambosasa
aliwataja wengine waliopoteza maisha kuwa ni Baruku Rashid (64), Mohamed Issa (67),
Stanlaus Joseph(68), Steven
Yessey (61), Monika Legukama (42), Alex
Madega (41), Hamis Mbala (35) na Ekson Nyoni (28), wote wakazi wa
Kimara.
Alisema watu hao waliwabaini baada ya kupata
taarifa kuwa, kuna watu wako Hospitali ya Mwananyamala na Tumbi, iliyopo Kibaha, ambao walifariki kwa kunywa gongo.
Pia, alisema miili ya watu hao imehifadhiwa katika
Hospitali ya Taifa, Muhimbili, ikitokea Hospitali ya Mwananyamala.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Daniel
Nkungu alilithibitishia gazeti hili kupokea miili hiyo tangu Jumanne, kwa
nyakati tofauti.
Alisema awali, alipokea miili saba huku baadhi
wakiwa bado wazima na wengine wamepoteza maisha. Alisema walioonekana wazima,
hawakuendelea kuishi muda mrefu, kabla ya kupoteza maisha.
"Hadi sasa tayari tumeshaipeleka miili hiyo
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi," alisema Dokta
Nkungu.
No comments:
Post a Comment