Friday, 6 October 2017

KIAMA UHAMIAJI, WAGENI WANAOISHI KISANII WATAKIWA KUJISALIMISHA





IDARA ya Uhamiaji nchini, imetoa siku 30 kwa raia wa kigeni wanaofanya kazi nchini kinyume cha utaratibu, kujisalimisha kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa.
Agizo hilo linawahusu wageni wanaofanya kazi nchini bila kuwa na vibali vya ukazi, hivyo kutakiwa kufika katika ofisi yoyote ya Uhamiaji kujisalimisha.
Kamishina wa Uhamiaji, Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka, Samweli Magweiga, alisema hayo jana, wakati akizungumza na vyombo vya habari mjini Dar es Salaam.
Alisema wale watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo, watatozwa  adhabu ya faini ya sh. 50,000 au kifungo cha miezi minane jela.
“Kwa mujibu wa kanuni ya 29(1),(2) na 30 za kanuni za Uhamiaji za mwaka 1997 na marekebisho yake ya mwaka 2016, chini ya sheria ya Uhamiaji sura ya 54, rejeo la mwaka 2002, inatoa masharti kwamba:
 “Wageni wote wenye vibali vya ukaazi, wanatakiwa kuripoti na kuwasilisha taarifa za anuani zao, zikiwemo mabadiliko kwa Kamishna Jenerali wa Uhamiaji na katika ofisi za uhamiaji, kwenye maeneo wanayoishi na kufanya kazi," alisema.
Magweiga aliwataka waajiri, wakiwemo wakurugenzi wa kampuni na taasisi mbalimbali, ambazo zina raia wa kigeni, kuhakikisha wanawahimiza waajiriwa kufika katika ofisi za Uhamiaji.
Alisema wako baadhi ya raia hao wa kigeni wamepata vibali vya kufanyakazi  katika ofisi za ajira nchini, lakini hawana vibali vya ukaazi, hivyo kuwataka nao kuitikia wito huo.
Aliwaasa wananchi kutoa taarifa kwa raia wa kigeni wanaowagundua kuwa hawana vibali vya ukaazi na kutoa taarifa kwa idara hiyo.
Pia, alisema watendaji wa vijiji na mitaa wanapaswa kutoa ushirikiano kwa idara hiyo, kwani raia hao ndiyo wanaoishi nao, hivyo wahakikishe wameripoti kwao.
“Kila changamoto ina fursa zake, suala la utambulisho wa raia wa kigeni la watu wote, wenye viwanda, kampuni, sheria hii inawasukumua waajiri na wananchi kutimiza wajibu wa kutoa taarifa za raia wa kigeni,”alisema.
Akizungumzia uhamiaji haramu nchini, alisema ni changamoto kubwa inayowakabili kutokana na wahamiaji hao kuwa katika makundi ya walowezi, utafutaji maisha na nchi kuwa njia ya kwenda nchi nyingine.
Kwa mujibu wa Kamishina Magweiga, raia wa nchi za Somalia na Ethiopia, ndiyo wanaokamatwa kwa kiasi kikubwa kujihusisha na uhamiaji haramu.
Pamoja na hayo, alisema hali ya uhamiaji haramu nchini siyo mbaya ya kutishia amani, ikilinganishwa na baadhi ya nchi duniani.
Agizo  la  idara hiyo, limekuja baada ya kutokea kwa baadhi ya matukio ya wahamiaji haramu, walioingia nchini kwa kupita au kuishi nchini kinyume cha sheria.
Juni 18, mwaka huu, wahamiaji 45, kutoka nchini Ethiopia, walikamatwa katika Kijiji cha Horohoro, wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga.
Kulingana na taarifa za idara hiyo, wahamiaji hao walikuwa safarini kuelekea nchini Afrika Kusini, walikamatwa baada ya kufichuliwa na raia wema.
Mbali na tukio hilo, Septemba 25, mwaka huu, raia wa Ethiopia wapatao 31, walikamatwa katika eneo la Tuangoma, Wilaya ya Temeke, kwa kuishi nchini bila ya kuwa na kibali.
Walifikishwa katika Mahakama ya Kisutu, huku kesi yao, ikiahirishwa hadi Oktoba 11, mwaka huu, kwa kusomewa maelezo ya awali.
Vivyo hivyo, mwaka jana, kipindi cha mwezi Januari hadi Novemba, wahamiaji 23,000, walikamatwa na idara hiyo kwa kuingia nchini kinyume na taratibu.
Kwa mujibu wa idara hiyo, lengo ni kutokomeza uhamiaji haramu nchini ili kulinda usalama wa nchi na mipaka yake.

No comments:

Post a Comment