Thursday, 5 October 2017
ZANZIBAR HAIJAMEZWA NDANI YA MUUNGANO-UDP
HATIMAYE Chama cha United Democratic Party (UDP), kimevunja ukimya na kusema kuwa, Zanzibar haijamezwa ndani ya Muungano kama inavyodaiwa na baadhi ya wanasiasa.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Juma Khamis Faki, amesema kama Zanzibar ingekuwa imemezwa, isingekuwa na Baraza la Wawakilishi, Katiba pamoja na vyombo vyake vya ulinzi.
Akizungumza na Uhuru, jana, mjini hapa, Juma alisema kauli za baadhi ya wanasiasa wanaodai kwamba, Zanzibar imemezwa ndani ya Muungano, hazina mashiko na zina lengo la kueneza chuki na fitna miongoni mwa wananchi na serikali yao.
Alisema nyingi zimeungana, lakini zimeshindwa kudumu kutokana na mikataba na makubaliano kukiukwa, hivyo kuwataka Watanzania kushikamana ili kuuenzi na kudumisha Muungano, ambao ni tunu ya Taifa.
“Kauli za kwamba Zanzibar imemezwa ndani ya Muungano, hazina mashiko kwani Zanzibar inacho chombo chake cha kutunga sheria, katiba, vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na bendera yake,”alifafanua.
Aliongeza kuwa, uwepo wa bendera ya Zanzibar kwenye Ofisi ya SMZ, ni ishara kwamba, Zanzibar ipo na kusisitiza bendera za SMT hupepea kwenye ofisi za Muungano pekee.
Alieleza kuwa sio jambo la busara kwa wanasiasa kuendelea kupandikiza mbegu, ambazo hazina nia njema kwa wananchi wa Zanzibar, bali wanatakiwa kuyatumia majukwaa ya siasa kuhubiri maendeleo.
“Ni vyema wanasiasa wakayatumia majukwaa ya siasa kuhubiri maendeleo na kuacha kupandikiza mbegu za chuki, ambazo zinaweza kuwafanya wananchi, hususan kizazi kipya, kuichukia serikali,”alieleza.
Amewataka wananchi kuwapuuza wanasiasa wanaotumia vibaya majukwaa na nafasi zao kupandikiza mbegu za chuki, badala yale waendelee kushirikiana kuudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment