Thursday, 5 October 2017
AFP: MAALIM SEIF NI WA PROPAGANDA
CHAMA cha Wakulima Tanzania (AFP), kimesema aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar, kupitia chama cha CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, amehusika kuidanganya dunia tangu mwaka 1995, akidai ameshinda uchaguzi kwa lengo la kusaka huruma ya kisiasa.
Kimesema Maalim Seif amekuwa akifanya hivyo kuwazubaisha wafuasi wake kwa propaganda ili waendelee kumwamini na kumpa nafasi zaidi.
AFP imesema kiongozi huyo ametumia nguvu nyingi kutafuta umaarufu wa kisiasa ili kujionyesha anakubalika huku akiidanganya dunia.
Shutuma hizo zilitolewa jana na Mwenyekiti wa Taifa wa AFP, Said Soud Said, alipozungumza na Uhuru, nyumbani kwake, Mbweni, nje kidogo ya Mji wa Unguja.
Soud alisema wananchi wa Zanzibar, Tanzania na Jumuia ya Kimataifa, zikiwepo nchi wahisani, wameshambaini mwanasiasa huyo kwamba, ni mbabaishaji na bingwa wa kutengeneza propaganda.
Alisema iwapo ameweza kuwadanganya wananchi, hususan wanachama wa chama chake, akidai ataapishwa na Umoja wa Mataifa, Septemba, mwaka huu,hicho ni kielelezo tosha kuwa mwanasiasa huyo ni hodari wa kudanganya.
"Ameanza kutoa madai ya kuibiwa kura za urais tangu mwaka 1995 hadi 2015. Hana ushahidi wala vielelezo. Mara hii ametoa kali aliposema ataapishwa na Umoja wa Mataifa (UN). Nadhani dunia sasa imemtambua na pengine itampuuza zaidi,"alisema.
Alisema yapo madai aliyowahi kuyatoa wakati wa mfumo wa chama kimoja, alipotaka kuteuliwa kuwa mgombea urais na kueleza kura zake halali alipewa Mzee Idris Abdul Wakil, jambo ambalo pia linaaoneka kuwa siyo la kweli, bali ulikuwa uzushi.
Mwenyekiti huyo wa AFP alimshutumu Maalim Seif, kwa kutoa madai ya aina hiyo hadi Jumuia ya Madola, chini ya aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Chifu Emeka Anyauko, mwaka 1999, kuanzisha mazumgumzo ya kusaka upatanishi wakati hakukuwa na uthibitisho wa kushinda kwake.
"Uongo siyo jambo linaloishi au kudumu kwa muda mrefu. Ameeneza propaganda nyingi huku akiiaminisha dunia anashinda uchaguzi. Kama angekuwa na nguvu za kidemokrasia za kushinda, nina hakika asingesusia uchaguzi wa marudio Machi 16, mwaka jana,"alieleza.
Akitoa mfano, alisema muungano wa NASA, nchini Kenya, chini ya mgombea wake wa urais, Raila Odinga, baada ya mahakama kufuta matokeo ya awali, ulikubali kuchuana tena na Jubilee, mbele ya mgombea wake, Rais Uhuru Kenyatta bila kugoma au kuleta longolongo.
Soud aliwataka Wazanzibari kuendelea na shughuli zao za kila siku za kujitafutia riziki, kujiongezea vipato kibiashara na kiuchumi, badala ya kuweka mikusanyiko ya kupeana hadithi na matumaini ya kuapishwa kwa Maalim Seif, jambo ambalo haliwezi kutokea bila kufanyika kwa uchguzi mkuu.
"Kwake hivi sasa jambo la maana angeshughulikia kupata ufumbuzi wa mgogoro wake na Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, aliyemsimisha kazi za utendaji. Aache kuwazuga wafuasi wake kwa maneno ya kutunga wakati nchi inaye rais kwa mujibu wa sheria na katiba,"alieleza Soud.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment