Thursday, 5 October 2017
'WANAMPINGA JPM NI WEZI, WALA RUSHWA'
MWENYEKITI wa TLP, Augustine Mrema, amesema baadhi ya watu wanaompinga Rais Dk. John Magufuli ni wale waliokuwa wala rushwa na wezi wa rasimali za taifa.
Pia, amsema kitendo cha kiongozi huyo kupambana na rushwa, ni kielelezo cha kutosha kwamba, rais ni mzalendo kwa nchi yake.
Akizungumza na gazeti hili, nyumbani kwake, maeneo ya Sinza jijini Dar es Salaam, juzi, alisema anawashangaa wanaopinga kazi anazofanya Rais Magufuli.
Alisema wanaoendelea kufanya hivyo, wamechanganyikiwa kutokana na wakati mgumu walio nao.
Mrema alisema, wanaobeza ni wale ambao mirija yao ya ufisadi, wizi na ubadhilifu, imezibwa na walizoea kuishi kwa njia za ujanja.
Alisema kwamba, kazi inayofanywa na rais ni nzuri, hivyo inapaswa Watanzania wamuunge mkono ili nchi isonge mbele.
"Huyu ni kiongozi tuliyeletewa na Mungu, unajua wapinzani tulikuwa tunapiga kelele kuhusu rushwa na rasilimali za taifa, kazi hiyo inafanywa vizuri na Rais Dk. Magufuli, ingawa wapo watu wanapinga.
“Kwa kweli, hawa ni wale waliokuwa wananufaika na wengine ni wezi," alisema.
Alisema Rais Magufuli ni kiongozi hodari, jasiri, mcha Mungu ambaye anatetea wanyonge kutokana na baadhi ya watu kuinyonya nchi kwa miaka mingi.
Mrema, alisema ataendelea kumuunga mkono Dk. Magufuli kwa vile kazi anayoifanya kulinda rasilimali za nchi, yakiwemo madini, naye aliwahi kujaribu kuifanya alipokuwa Naibu Waziri Mkuu miaka iliyopita.
"Viongozi wote waliopita wamefanya kazi nzuri, lakini hata mimi nilipapasa kidogo mambo ya madini na kukamata pale uwanja wa ndege, sasa huyu Rais, ameweka nguvu na faida tutaiona kwa vile hivi sasa wizi wa madini hakuna tena,"alisema.
Mwenyekiti huyo wa TLP, aliongeza kwamba, kazi hiyo ni kubwa, inabidi wananchi wamuunge mkono ili baadae nchi nzima iweze kunufaika.
"Ukweli nasema, angalia amefufua Shirika la Ndege ATCL, bado amedhibiti wizi wa fedha za serikali kwa wafanyakazi hewa, wanafunzi hewa, sasa tunajenga reli yetu ya kisasa ya treni 'Standard Gauge,' kwa fedha zetu, tunapaswa tumuunge mkono, haya ni mafanikio makubwa," alisema Mrema.
Akizungumzia kuhusu hali ya kisiasa, Mrema alisema ni nzuri licha ya kuwepo kasoro chache ambazo zinaweza kuzungumzika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment