WATU wawili wanashikiliwa na polisi mkoani hapa, kwa
tuhuma za kumtaka mkono mtu mwenye ulemavu wa ngozi katika kijiji cha
Nyarutanga, Kata ya Kisaki, Wilaya ya Morogoro.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonce
Rwegasira, alisema jana kuwa, tukio hilo lilitokea Oktoba 3, mwaka huu, saa
6.00 usiku.
Alisema watu wasiojulikana, walivamia nyumba ya Nassoro
Msingili (75), mkazi wa kijiji hicho, ambaye ana ulemavu wa ngozi, kisha
kumkata mkono.
Kamanda huyo alisema, Msingili akiwa amelala chumbani,
alivamiwa na watu hao, akakatwa mkono wa kushoto na baada ya tukio hilo,
walitokomea kusikojulikana.
Alisema majeruhi huyo amelazwa katika Kituo cha Afya
Duthumi, akipewa matibabu, lakini hali yake siyo nzuri.
Kamanda huyo alisema juhudi za kuwatafuta waliofanya
uhalifu huo zinaendelea, ambapo tayari watu wawili, ambao hakutaja majina yao,
wanashikiliwa.
Alisema polisi inapinga vikali mauaji ya kikatili yanayofanywa
kwa watu wenye ulemavu wa ngozi na kuahidi waliohusika kusakwa kwa nguvu zote.
Katika hatua nyingine, kamanda huyo aliwataka wananchi
wanaoishi jirani na watu wenye ‘albinism,’ wawe na mazoea ya kuwalinda ili
kuepusha na madhara yoyote ya maisha yao.
No comments:
Post a Comment