WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amepiga marufuku tabia ya
baadhi ya viongozi katika maeneo mbalimbali nchini, kuwakamata na kuwaweka
mahabusu watumishi, wakiwemo wauguzi bila kufuata utaratibu.
Pia, amewataka wauguzi nchini, kufanya kazi kwa weledi,
uaminifu na kufuata maadili ya taaluma yao kwa kuwa maisha ya wagonjwa yako
mikononi mwao.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana, wakati akifunga Mkutano
Mkuu wa Mwaka wa 45 wa Chama cha Wauguzi Tanzania, mkoani Lindi.
“Naagiza viongozi wote kufuata na kuzingatia sheria. Kama
kuna makosa ya kitaaluma, mabaraza husika yashughulikie jambo hilo, ni marufuku
kuwaweka ndani watumishi kwa tuhuma za kitaaluma,”aliagiza.
Alisema katika sekta ya afya, bila wauguzi ambao ni
kundi kubwa kati ya wanataaluma wa afya, serikali haitaweza kutekeleza ipasavyo
mikakati mbalimbali iliyopangwa.
Aidha, Waziri Mkuu aliwaasa wauguzi wote nchini,
kuhakikisha wanazingatia kiapo cha maadili ya kazi yao na kwamba, serikali
haitamvumilia yeyote atakayebainika kwenda kinyume.
Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha afya za Watanzania
wote zinaimarika ili kuendana na kasi ya utendaji kazi ya kuinua uchumi na
kufikia kiwango cha kati, hivyo ni lazima watoe huduma bora kwa wananchi.
Pia, amewaomba waunge mkono kwa nguvu zote jitihada za serikali
kuhakikisha miundombinu na vifaa vyote, havihujumiwi na wachache ili viwe
msaada mkubwa, hususani kwa kinamama wajawazito.
Akizungumzia kuhusu upungufu wa wauguzi nchini, Majaliwa alisema serikali itaendelea kuajiri watumishi
wa kada mbalimbali, wakiwemo wauguzi na wakunga na kuwapanga katika maeneo
yenye upungufu zaidi.
Awali, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Dk. Khamis Kigwangalla, alisema baadhi ya viongozi katika
maeneo mbalimbali nchini, wamekuwa wakiwakamata na kuwachukulia hatua watumishi
wa sekta ya afya bila kufuata utaratibu, jambo ambalo siyo sahihi.
No comments:
Post a Comment