Thursday 5 October 2017

UCHAGUZI WA MADIWANI KATA 43 KUFANYIKA NOVEMBA 26




TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetangaza uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 43, utakaofanyika Novemba 26, mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa jana, kwa vyombo vya habari na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage, ilisema uchaguzi huo unafanyika kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo baadhi ya madiwani kufariki  dunia.
Alizitaja sababu zingine kuwa ni baadhi ya madiwani kujiuzulu, kutohudhuria vikao na wengine ushindi   wao kutenguliwa na mahakama.
Mwenyekiti huyo alizitaja kata hizo na mikoa kuwa ni  Arusha (Musa, Muriet, Ambureni, Ngabobo, Maroroni, Leguruki, Makiba na Moita), Dar es Salaam (Mbweni, Kijichi na Saranga).

Zingine ni Dodoma (Chipogolo), Geita (Bukwimba na Senga), Iringa ( Kitwiru na Kimala), Kilimanjaro (Bomambuzi, Mnadani, Machame Magharibi na  Weruweru), Lindi (Chikonji na Mnacho).

Kata zingine ni Manyara ( Nangwa), Mbeya (Ibighi),  Morogoro (Kiloka na Sofi),  Mtwara ( Milongodi,  Reli na Chaninguo), Mwanza ( Kijima na  Mhandu), Rukwa ( Sumbawanga), Ruvuma   (Lukumbule, Kalulu na Muongozi) na Singida (Siuyu).

Zingine ni Simiyu (Nyabubinza), Songwe ( Dalambo),  Tabora ( Nata na Muungano) na  Tanga ( Majengo, Lukuza na Mamba).

Jaji  Kaijage  alisema, wameamua kutangaza uwepo wa uchaguzi huo, baada  ya waziri  mwenye dhamana ya serikali  za mitaa  kuwataarifu uwepo wa nafasi wazi za madiwani katika  kata hizo zilizoko  katika  halmashauri   36, kwenye mikoa 19 ya Tanzania Bara.
Alibainisha kuwa kifungu cha 13 (1) cha Sheria  ya Uchaguzi ya Serikali  za Mitaa, Sura  ya 292, kinampa mamlaka  waziri  mwenye dhamana ya serikali  za mitaa, kutoa taarifa kuhusu kuwepo kwa nafasi  wazi  za  madiwani katika  kata husika.
Jaji Kaijage alisema  baada  ya kupokea taarifa  hiyo  na kwa  kuzingatia masharti ya kifungu  cha 13(3) cha Sheria  ya Uchaguzi ya Serikali  za Mitaa, wana wajibu wa kuitisha na  kuendesha uchaguzi mdogo katika kata hizo.
Alisema   ratiba   ya  mchakato  wa   uchaguzi  huo   inatarajia kuanza Oktoba 26, mwaka huu, ambapo  kutafanyika uteuzi  wa wagombea udiwani na kampeni zitaanza Oktoba  27 na kumalizika Novemba 25, mwaka.
Jaji Kaijage alitoa wito kwa vyama  vya  siasa  na  wadau   wote  wa  uchaguzi,  kuzingatia matakwa  ya   Katiba,  Sheria   ya   Uchaguzi  ya  Serikali   za   Mitaa,   Kanuni   za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Madiwani) za mwaka  2015.
Pia, maadili ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2015, pamoja na maelekezo yote yaliyotolewa au yatakayotolewa na  NEC wakati  wa  uchaguzi  huo.

No comments:

Post a Comment