Thursday 5 October 2017

WASOMI WAICHAMBUA MIAKA MIWILI YA RAIS MAGUFULI MADARAKANI




NA WILLIAM SHECHAMBO
UKIWA umesalia mwezi mmoja kwa Rais Dk. John Magufuli kutimiza miaka miwili madarakani, wadau kutoka sekta mbalimbali nchini, wamesema anakwenda vizuri.
Kauli hiyo, imeambatana na zingine kwamba, wameridhishwa na mwenendo wa serikali ya awamu ya tano na endapo ushirikiano utaendelezwa, baina ya serikali na watumishi wa umma na sekta binafsi, mambo yataendelea kuwa mazuri zaidi.
Wakizungumza na Uhuru, kwa nyakati tofauti jana, wamesema Novemba 5, mwaka 2015, Rais Dk. Magufuli alipokula kiapo kuwatumikia Watanzania mpaka kufikia leo, Oktoba 5, mambo mengi, yamefanyika.
Profesa Joseph Mbwiliza wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), alisema miaka miwili ya Rais Magufuli, imekuwa na mafanikio mengi na changamoto kadhaa, ambazo kama ilivyo barabara kukosa kona na bahari kukosa mawimbi, hazikosekani kwenye utendaji wowote.
Alisema Dk. Magufuli aliipokea nchi ikiwa na utulivu na amefanikiwa kuutunza, kutokana na hofu ya Mungu aliyonayo na maombi, ambayo kila anaposimama kuzungumza, huwaomba Watanzania wamuombee.
Profesa huyo wa Sayansi za Siasa na Mkuu wa Chuo wa zamani wa Chuo cha Mwalimu Nyerere (Magogoni), alisema katika masuala ambayo ameyaona yamefanikiwa na yana umuhimu kwenye serikali ya sasa, ni ukusanyaji kodi.
Alisema kodi kwenye maendeleo ya taifa lolote ni muhimu na kwamba, ni aibu kwa mtu kulalamika pale anapotakiwa kulipa kodi, kwa sababu ni lazima kwa maendeleo yake na taifa lake kwa ujumla.
Profesa Mbwiliza alisema, linalotia moyo ni namna ambavyo serikali hiyo imeweka umakini katika matumizi ya fedha hizo za kodi ya wananchi, suala ambalo ni akili ya kiasi cha juu kwa maslahi ya taifa.
Pia, alisema changamoto zinazotajwa kwenye uongozi wa Rais Magufuli, hazitakiwi kuondoa imani ya wananchi kwake, kama ilivyo kwa abiria kutoshauriwa kuacha kumwamini dereva kwa sababu nchi itayumba na hasara itakuwa ya Watanzania.
"Hata kwenye familia, hata kama watu wanapendana vipi, siku zote haziwi sawa, hii nchi inakwenda kwa misingi ya sheria, hakuna linaloshindikana kwenye mazungumzo," alisema.
Aliongeza kuwa Rais Magufuli amefanikiwa kuonyesha njia ya kwenda kama taifa, hivyo kila Mtanzania anapaswa kuifuata kwa sababu ni safari njema, lakini yenye kona na mawimbi yanayohitaji mshikamano na kujituma ili kufika salama.
"Rais kwenye kipindi hiki tangu aingie madarakani, amefanikiwa kuonyesha dira, hajajali kukosa misaada ya wahisani, bali kufanya kila linalotakiwa kufanywa kwa maslahi ya taifa hili, hivyo anapaswa kuungwa mkono," alisema.
Mwalimu Honoratha Chitanda, aliyekuwa Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), alisema licha ya kuwa mstaafu, anapongeza kazi kubwa iliyofanywa kwenye kuwaondoa watumishi hewa.
Alisema alipokuwa kwenye utumishi wa umma na kiongozi wa CWT, suala la watumishi hewa walilizungumzia kwa muda mrefu, kwa kuwa uwepo wake ulikuwa ukiwanyonya watumishi halali, hususan kwenye suala la stahiki zao kimaslahi.
Honoratha alisema, serikali kama alivyoeleza Rais Magufuli juzi, kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa 33 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT), ilikuwa ikitumia kiasi kikubwa cha fedha kwa mishahara.
Dk. Magufuli kwenye mkutano huo alisema, awali kabla ya msako wa watumishi hewa, takriban sh. bilion saba, zilikuwa zikilipwa na serikali kila mwezi kwa ajili ya mishahara ya watumishi na baada ya 'usafishaji', fedha hizo zimeshuka mpaka takriban sh. bilioni mbili.

Honoratha alisema mzigo huo wa malipo ulisababisha mkwamo kwenye ulipaji wa maslahi ya watumishi, hususan walimu, ambao wanachukua sehemu kubwa ya watumishi wa umma kutokana na wingi wao.
Mwalimu huyo mstaafu alifafanua kuwa, madeni makubwa ya serikali kwa watumishi wa umma, yakiwemo malimbikizo ya mishahara, yasingefika kiasi kilichofikia kama watumishi wote wangekuwa halali.
"Pamoja na mengi yaliyofanywa, nazungumzia kwa nafasi yangu kwamba, kuondolewa kwa watumishi hewa ni jambo kubwa zaidi kufanywa na serikali hii ya Dk. Magufuli," alisema.
Aliongeza kuwa, kwa sababu suala hilo limefanikiwa huku serikali ikiahidi kuendelea nalo kwa udhibiti zaidi, inapaswa ikaanza kuboresha maslahi ya watumishi wa umma.
"Sasa hivi watumishi wa umma ni wachache, fedha nyingi zimeokolewa na wana mzigo mkubwa, hivyo ni vema wakaangaliwa kwa jicho la tatu kwenye ulipaji wa madai yao.
"Ajira pia kwa kuwa zimesimama kwa muda mrefu kupisha ukaguzi wa watumishi hewa na vyeti vya kughushi, ahadi ya kuajiri itekelezwe kwa vitendo ili utumishi wa umma ushike hatamu," alisema.
Fahmi Dovutwa, ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha United People's Democratic Party (UPDP), alisema miaka miwili ya Rais Magufuli itaacha alama ya uongozi makini wenye kujali maslahi ya Watanzania.
Alisema jambo la kufariji ni kuona sasa Watanzania wanyonge wana sauti pale wanapokuwa wameonewa na watu waliojifanya miungu watu katika awamu zilizopita za serikali.
Dovutwa alisema suala la kudumisha amani na utulivu wa nchi, hakuna anayeweza kulipinga kwa sababu hata pale kulipotokea kundi lililotaka kuharibu amani, chini ya uongozi wake, serikali ilisimama kidete kupambana nalo.
Kiongozi huyo wa UPDP aliongeza kuwa, katika miaka miwili ya Dk. Magufuli madarakani, migogoro ya ardhi imedhibitiwa na kutatuliwa kwa kiasi kikubwa, tofauti na hali ilivyokuwa miaka 10 iliyopita.
Mbali na hayo, alisema kama mwanasiasa, amefarijika kwa uamuzi wa serikali kupiga marufuku mikutano ya hadhara ya kisiasa, kwa sababu ilikuwa ikivikandamiza baadhi ya vyama vya siasa hapa nchini.
Alisema awali, Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, alisema vyama vya siasa vyote vilikuwa sawa kwenye suala la kupewa ruzuku, lakini baadaye utaratibu ulivurugika kwa uwepo wa sheria namba 11 ya mwaka 1996.
"Kuanzia hapo, vyama vyenye wabunge ndio vilipewa ruzuku, sasa vile vya upinzani vinatumia fedha hizo kufanya mikutano na kuvitukana vyama vidogo, hili lilituumiza sana kwa muda mrefu.
"Sasa ndani ya miaka hii miwili wote tupo sawa, hakuna kutukanana na kukandiana kwenye majukwaa kama ilivyokuwa awali. Walisema Dovutwa CCM, mara ooh...kibaraka na kadhalika... Tukutane 2020, tuone nani anajua siasa," alifafanua.
Novemba 5, mwaka huu, Rais Dk. Magufuli atatimiza miaka miwili ya kuwa madarakani baada ya kuapishwa tarehe kama hiyo mwaka 2015, kufuatia kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa mshindi wa kiti cha urais kwa tiketi ya CCM, kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015.

No comments:

Post a Comment