Thursday 5 October 2017

BONDE LA EYASI WEMBERE LAONYESHA DALILI ZA UWEPO WA MAFUTA


TIMU ya wataalamu kutoka Uganda na Tanzania, wakiwa katika miamba inayoonekana katika kijiji cha Mwanzugi, wilayani Igunga, ikiwa ni maandalizi ya shughuli za utafiti wa mafuta katika Bonde la Eyasi Wembere na Ziwa Tanganyika.


Na Teresia Mhagama, Tabora

MIAMBA iliyoko katika Bonde la Eyasi Wembere, hususan mabonde madogo (sub basin) ya Wembere na Manonga, yaliyoko katika mikoa ya Tabora, Shinyanga, Singida na Simiyu, inawezekana kuwa na mafuta kutokana na sifa zake za Kijiolojia na Kijiofizikia.

Hayo yameelezwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini (Uganda), Robert Kasande na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini (Tanzania), Dk. Mhandisi Juliana Pallangyo, katika mkutano na wananchi, uliofanyika juzi, katika kijiji cha Mwashiku, wilayani Igunga, mkoani Tabora. Mkutano huo uliandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry.

Viongozi hao walitoa kauli hiyo baada ya timu ya wataalamu kutoka Uganda na Tanzania, kufanya ziara katika bonde hilo, hususan mabonde madogo ya Wembere na Manonga na kutembelea miamba inayoonekana katika maeneo ya Sekenke mkoani Singida na vijiji vya Mwanzugi na Kining'inila, mkoani Tabora.

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, alieleza kuwa baada ya kuona dalili hizo, timu hiyo itatoa mapendekezo mbalimbali kwa wataalamu wa Tanzania, ili kuweza kufikia lengo la serikali la kuchimba mafuta katika Bonde la Eyasi na Ziwa Tanganyika .

Alisema endapo mafuta yatapatikana katika bonde hilo, yataweza kusafirishwa katika bomba la mafuta linalotoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga na kuuzwa ndani na nje ya nchi.

Aliongeza kuwa, kuna uwezekano mkubwa kwa Tanzania kugundua mafuta katika bonde hilo, kwani nchini nyingine, ambazo linapita kama vile Kenya na Uganda, tayari wamegundua mafuta.

Naibu Katibu Mkuu, Dk. Mhandisi Juliana alisema kupatikana kwa mafuta katika eneo hilo, kutaimarisha hali ya uchumi nchini na kuwaasa wananchi kujiandaa na fursa za kiuchumi, ikiwemo utoaji wa huduma mbalimbali wakati wataalamu hao wakiwa wanafanya shughuli mbalimbali za kitafiti katika eneo husika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry aliwataka wananchi wanaozunguka bonde hilo na viongozi wa serikali katika mkoa huo, kutoa ushirikiano kwa wataalamu watakaofanya kazi za kitafiti ili zoezi hilo liweze kufanyika kwa ufanisi.

Mjiofizikia kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Sindi Maduhu, alisema bonde hilo la Eyasi Wembere, lina ukubwa wa kilomita za mraba 19,197, likiwa na takwimu za awali za kijiofizikia (Airborne gravity gradiometry) zilizokusanywa na kutafsiriwa mwaka 2015/2016.

No comments:

Post a Comment