Wednesday 4 October 2017

LEMA, NASSARI, MSIGWA WAINGIA MITINI TAKUKURU



 
WABUNGE watatu wa CHADEMA, jana waliingia mitini na kushindwa kuwasilisha ushahidi zaidi wa tuhuma za rushwa kwa madiwani 10, waliojiuzulu chama hicho.

Juzi, wabunge hao waliwasilisha baadhi ya vielelezo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Valentino Mlowola, wakidai kuwa ni ushahidi dhidi ya madiwani hao.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo wa TAKUKURU, aliwaagiza wabunge hao kuwasilisha vielelezo zaidi kuhusu tuhuma hizo dhidi ya wabunge hao jana, lakini walishindwa kufanya hivyo.

Hayo yalibainika baada ya wabunge hao, Joshua Nassari (Arumeru Mashariki), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Mchungaji Peter Msigwa wa Iringa Mjini, kushindwa kuonekana kwenye ofisi za makao makuu ya TAKUKURU, Dar es Salaam, kama walivyowaahidi waandishi wa habari.

Juzi, walipofika kwenye ofisi hizo ili kuwasilisha ‘flash’ waliyodai kuwa na video za ushahidi wa viongozi wa serikali kupanga njama za kuwanunua madiwani hao, waliahidi wangefika tena jana, ili pamoja na mambo mengine kufungua jalada la upelelezi huo.

Uhuru jana, liliweka kambi maeneo ya Upanga, mpaka muda wa kufunga ofisi za serikali, bila kuona dalili za ujio wa wabunge hao waliojitamba kwa wanahabari mkoani Arusha kwamba, wanao ushahidi wa kutosha juu ya madai yao.

'Kukacha' kwao kulithibitishwa na Msemaji wa TAKUKURU, Mussa Misalaba, ambaye alisema bado wanaendelea kuwasubiri viongozi hao kwa ajili ya kuwasilisha ushahidi zaidi, kwa kuwa video pekee haitoshi kukamilisha uchunguzi na kutoa haki kwa anayestahili.

"Niko nje ya ofisi, lakini bado uchunguzi wa tuhuma hizo unaendelea. Waheshimiwa wabunge bado tunawasubiri watuletee ushahidi zaidi kwa kuwa hii video haitoshi na bila ushahidi zaidi haina maana," alisema Misalaba.

Aliongeza kuwa, sababu ya TAKUKURU kudai ushahidi zaidi ni kutokana na uwepo wa mambo mengi kwenye madai yao na taratibu za uchunguzi wa taasisi hiyo zinazohitaji ushahidi wa kutosha.

Mbali na hilo, Misalaba alisisitizia kauli ya Mkurugenzi wake mkuu, Mlowola, ambayo aliitoa juzi, kwa wabunge hao kuwa uchunguzi utafanywa kwa weledi mkubwa bila kujali upande wa viongozi hao kisiasa.

Uhuru kwa uchunguzi wake wa kuaminika, lilipata utetezi wa Nassari kuhusu kutokuonekana kwao kwenye ofisi za TAKUKURU jana, kwamba walikuwa wanasubiri 'vitu fulani' kabla ya kurudi tena ofisini hapo leo.

Wiki iliyopita, Nassari na  Lema walikutana na wanahabari na kuonyesha video waliyodai kuwa ni ushahidi wao juu ya tuhuma kwamba, madiwani waliokuwa CHADEMA na baadaye kujiuzulu, walinunuliwa.

Tuhuma hizo walizielekeza kwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti, Katibu Tawala wake, Timothy Mnzava na madiwani husika waliojiuzulu na baadaye kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Madiwani hao na kata zao kwenye mabano ni Edward Sepunyo (Moita), Manda Ngoitiko (Viti Maalumu), Rayson Ngowi (Kimandolu), Credo Kifukwe (Muriet), Solomon Laizer (Ngabobo), Anderson Sikawa (Leguruki), Emmanuel Mollel (Makiba), Bryson Isangya (Maroroni) na Josephine Mshiu wa viti maalumu.

Baada ya kujiuzulu, madiwani hao walitangaza kujiunga na CCM, ambapo Rais Dk. John Magufuli, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, aliwapokea na kuwakabidhi rasmi kadi za uanachama, akiwa kwenye ziara yake mkoani Arusha.

No comments:

Post a Comment