Tuesday 20 June 2017

BUNGE LAPITISHA BAJETI KWA KISHINDO, WABUNGE WACHACHAMAA WATAKA WAPINZANI WALIOPIGA KURA YA KUIKATAA BAJETI WASIPELEKEWE FEDHA ZA MAENDELEO


WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania, wameiomba serikali izuie fedha za maendeleo kwenda kwenye majimbo ya wabunge wa upinzani waliopiga kura ya hapana wakati wa kupitisha bajeti.

Wametoa pendekezo hilo wakati huu, ambapo Bunge limepiga kura kwa ajili ya kupitisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018.

Wabunge waliotoa pendekezo hilo ni pamoja na Jenista Mhagama, Hawa Ghasia, Amina Mollel, Joseph Msukuma, Charles Kitwanga na George Simbachawene.

Wamesema inashangaza kuona kuwa, wabunge takriban wote wa upinzani wamepiga kura ya kuikataa bajeti hiyo, wakati kwenye bajeti zimetengwa fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi katika majimbo yao.

Wamesema ni vyema ufike wakati serikali izuie fedha za maendeleo kwenda kwenye majimbo ya wabunge hao kwa sababu maamuzi yao yanawakosesha haki wananchi waoi.

Wamesema katika majimbo yanayoongozwa na wapinzani, wapo wananchi wa vyama vingine na wale ambao hawana vyama, hivyo kuipinga bajeti ya serikali ni kuwakosesha haki zao za msingi.

Wakati wabunge hao wakitoa miongozo hiyo kwa Spika Job Ndugai, wabunge wa CCM walishangilia kuonyesha kuwaunga mkono huku  wale wa upinzani wakionekana kunywea.

Mbunge wa Ukonga kupitia CHADEMA, George Waitara alijikuta akitolewa nje ya bunge na Spika Ndugai kutokana na kukataa kukaa kimya wakati wenzake walipokuwa wakizungumza.

Katika kupitisha bajeti hiyo, wabunge waliokuwepo ukumbini ni 356, waliopiga kura ni 355, kura za hapana 65 na kura za ndio 260. Bajeti hiyo imepitishwa kwa asilimia 72.

No comments:

Post a Comment