Tuesday, 22 August 2017
VIONGOZI WAKUU SCCULT WATUMBULIWA
MRAJISI Msaidizi wa Vyama vya Ushirika nchini, Tito Haule, amewasimamisha kazi viongozi wa Muungano wa Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SCCULT), ili kupisha uchunguzi wa ubadhirifu na upotevu wa mamilioni ya fedha za wana ushirika nchini.
Pia, mrajisi ameunda timu itakayofanya uchunguzi dhidi ya ubadhirifu huo, ambayo inaanza kazi mara moja.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, jana, Mrajisi Haule alisema uamuzi huo ulifikiwa kutokana na mkutano mkuu maalumu wa wanachama wa SCCULT, uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP).
Haule alisema taarifa ya ukaguzi, iliyowasilishwa katika mkutano huo, ndiyo iliyobaini madudu hayo na kuainisha hasara inayotokana na matumizi mabaya ya fedha za mikopo ya wanachama kutoka taasisi za mikopo.
“Kuna ubadhirifu mkubwa kwani hata katika taarifa yao ya utekelezaji ya kipindi cha 2016/2017, inaonyesha jinsi ambavyo matumizi yao ni makubwa kuliko kiasi cha fedha walichokusanya, ina maana wamewaibia na kula fedha za wanachama,”alisema Haule.
Mrajisi huyo aliongeza kuwa, viongozi wote waliosimamishwa, wanapisha uchunguzi na kazi hiyo inaanza mara moja na itakapokamilika, watachukuliwa hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Awali, akifungua mkutano huo, Kaimu Mrajisi huyo alisema alibaini kuwepo kwa utendaji usioridhisha wa SCCULT na kusababisha kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wanachama.
“SCCULT ilianzishwa kwa lengo la kuwaunganisha na kusimamia shughuli za ushirika katika maeneo mbalimbali, lakini cha kushangaza utendaji wake umekuwa ukileta malalamiko mengi,”alisema.
Haule aliongeza kuwa, tangu mwaka 2008, uendeshaji wake umekuwa siyo wa kuridhisha na kusababisha vyama wanachama kushindwa kupata huduma kutoka SCCULT.
Alifafanua kuwa, tangu alipoteuliwa Oktoba, 2016, amekwishapokea barua za SACCOS zenye malalamiko juu ya SCCULT na kwamba, baadhi ya malalamiko yalieleza kuhusu suala la akiba na hisa za vyama hivyo zilizowekezwa SCCULT kutojulikana zilipo.
Mrajisi huyo alitaja lalamiko jingine kuwa ni baadhi ya vyama kila mara vinapotaka kujitoa SCCULT, huwa hawapati fedha zao zilizowekezwa.
“Katika hayo, pia baadhi ya vyama vilikuwa vikilalamikia kutofanyika kwa mikutano na kutojulikana kwa taarifa za hesabu za chama chao kwa muda wa miaka minne sasa,”alisema.
Alisema baada ya kupokea malalamiko hayo, licha ya jitihada zilizokuwa zikiendelea katika ofisi yake kufuatilia utendaji wa SCCULT, aliamua kuiandikia barua SCCULT ili kupata taarifa za mkutano mkuu wa mwaka huu na makisio ya mapato na matumizi yaliyoandaliwa na chama hicho, ili aweze kujiridhisha na hali ya uendeshaji, lakini hakuweza kuzipata taarifa hizo.
Haule alifafanua kuwa baada ya kukosekana kwa taarifa hizo, ndipo alipoamua kuitisha mkutano mkuu maalumu wa wanachama na kwamba, SCCULT ilikuwa ikisimamia fedha za mifuko mbalimbali.
Akizungumza katika mkutano huo, Mtendaji Mkuu wa SCCULT, Habib Mhezi, alisema wameweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto hizo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment