Tuesday, 22 August 2017

LISSU SASA AWA 'NDEGE WA SELO'


POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imemtia mbaroni Mbunge Tundu Lissu (Singida Mashariki - CHADEMA), baada ya gari lake kuzingirwa mbele na nyuma, akiwa anatoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Lissu, ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa chama hicho, alitiwa mbaroni jana, saa 7.15 mchana, muda mfupi baada ya kutoka mahakamani hapo, alipokuwa akimtetea mshitakiwa Yericko Nyerere.

Mbunge huyo alifika mahakamani kuhudhuria kesi ya mshitakiwa Yericko, iliyokuwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbrad Mashauri.

Baada ya shauri hilo kuahirishwa, Lissu alisimama kwa muda katika viunga vya mahakama hiyo, akibadilishana mawazo na mawakili na watu wengine na baadaye aliingia kwenye gari lake aina ya Toyota Land Cruiser, lenye namba T 216 DHH.

Gari la Lissu lilianza kutoka katika viwanja vya mahakama hiyo huku gari la polisi, ambalo mbele alikuwepo Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kati, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Dennis Mujumba,lililokuwepo mahakamani hapo muda mrefu, lililifuata gari hilo kwa nyuma.

Hata hivyo, safari ya Lissu iliishia kwenye lango la kuingia na kutokea kwenye mahakama hiyo, baada ya gari lingine la polisi lenye namba RX04 EZN Toyota Landcruiser, lilipolizuia gari la mbunge huyo kwa mbele.

Baada ya kufanikiwa kulizuia gari hilo la Lissu, maofisa wa polisi waliokuwa wamevalia nguo za kiraia, walimfuata mbunge huyo aliyekuwa akiendeshwa na kumtaka ashuke kwenye gari, apande gari lao.

Wakati hayo yanatokea, Wakili Peter Kibatala, anayemwakilisha Lissu kwenye kesi zinazomkabili mahakamani hapo, ambaye alikuwemo ndani ya gari lake tayari kwa kuondoka, alikazimika kushuka na kumfuata mbunge huyo.

Kibatala alienda kuongea na Lissu, ambaye aliamua kutii amri ya polisi na kwenda kupanda kwenye gari lililokuwa limemzuia kwa mbele.

Nje ya ukuta wa mahakama hiyo, kulikuwa na gari jingine la polisi, likiwa na askari wenye silaha, ambapo baada ya kumtia mbaroni mbunge huyo, msafara wa magari manne, likiwemo la Lissu uliondoka.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni, alikiri kushikiliwa kwa Lissu.

"Ni kweli tunamshikilia  Lissu na sababu ya kukamatwa kwake, atakayetolea  ufafanuzi ni Kaimu Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam," alisema.

Kaimu Kamishna wa  Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya, alisema hajapata taarifa ya kukamatwa kwa Lissu.

"Nimetoka kwenye kikao kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul  Makonda na nimefika ofisini  muda ukiwa  umeenda, bado sijapata taarifa ya kukamatwa kwake, nikipata nitawaita kwa ajili ya kutolea ufafanuzi wa kina,"alisema Mkondya.

No comments:

Post a Comment