Tuesday, 22 August 2017

UINGEREZA YAPONGEZA SERA YA ELIMU BURE


SERIKALI ya Uingereza imeeleza namna ilivyovutiwa na mabadiliko yaliyofanywa kwenye sekta ya elimu nchini, kupitia sera ya elimu bure, ambayo imewezesha kuwepo kwa ongezeko kubwa la udahili kwa wanafunzi.

Kufuatia mabadiliko hayo, Uingereza imetoa paundi milioni 140, kusaidia maboresho kwenye miundombinu ya utoaji elimu, hususan ujenzi wa madarasa na nyenzo za ufundishaji.

Pia, nchi hiyo imeridhishwa na namna ambavyo serikali inavyopambana katika ulinzi wa maliasili, ikiwemo mapambano dhidi ya ujangili.

Akizungumza Dar es Salaam, jana, Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika nchini Uingereza, Stewart Rory, alisema baada ya kuwasili nchini, hatua ya kwanza alitembelea shule za msingi.

“Nimeshuhudia mabadiliko makubwa yaliyofanyika, ikiwemo utoaji elimu bure. Tutatoa zaidi misaada kusaidia masuala ya kitaaluma, ikiwemo ujenzi wa madarasa,” alisema.

Waziri Rory pia alieleza namna Uingereza inavyoridhishwa na juhudi za serikali katika kukabiliana dhidi ya majangili.

Alisema licha ya changamoto za umasikini, Tanzania imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha maliasili zilizopo zinaendelea kutunzwa kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga, alisema Uingereza ni nchi ya kwanza inayoongoza katika kutoa misaada ya kimaendeleo kwa Tanzania.

Alibainisha kuwa, nchi hiyo imeonyesha dhamira ya kuendelea kuisaidia Tanzania, hususan kwenye afya, maji, miundombinu, vita dhidi ya dawa za kulevya na ujangili.

Rory yupo nchini kutembelea miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Uingereza (Department for International Development – DFID).

Baadhi ya miradi hiyo ni upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Shule ya Msingi Mkoani, Bonde la Mto Msimbazi, Kiwanda cha Nguo cha Tooku, kilichoko eneo la viwanda la Benjamin Mkapa na Kampuni ya Songas.

No comments:

Post a Comment