MWANASHERIA Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu amedaiwa ni kibaraka
anayetumia siasa katika kuganga njaa, hivyo anapaswa kupuuzwa kwa kuwa uchoyo
unamfanya kutokuwa na uzalendo kwa taifa.
Lissu, ametajwa kuwa ni miongoni mwa wanasiasa wanaoshirikiana
na moja ya kampuni ya mawakili kuhujumu utendaji wa Shirika la Ndege Tanzania
(ATCL).
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Zanzibar,
Mohamed Ahmada Salum, akiwa na Kamati ya
Baraza la Wawakili ya Ardhi na
Mawasiliano, alisema jana kuwa, Lissu ni
kibaraka anayeumia na choyo, hivyo kutokuwa na
uzalendo kwa taifa.
Alisema Tanzania itajengwa na wananchi, hivyo ni vizuri kuwa
watulivu na kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli, katika kufanikisha uchumi wa
kati.
Mohamed alisema hatua ya hivi karibuni ya Lissu kuibuka katika
vyombo vya habari na kuonyesha furaha kwa kutokufika kwa ndege mpya ya tatu
aina ya Bombadier Q 400, ni choyo ya mafanikio.
Alisema Serikali ya
Zanzibar ilikutana na uongozi wa ATCL na kuridhishwa na hatua ya utekelezaji wa
majukumu yake, ikiwemo ujio wa ndege
hizo.
"Hakuna wa kuikomoa serikali, Lissu anatumia siasa kutaka
kuwachelewesha wananchi kufikia malengo na hawezi kufanikiwa. Tunajua
kinachomsumbua ni choyo na njaa na kutokuwa na elimu ya siasa ya uzalendo.
“Ukiona mwanasiasa yupo tayari kuhatarisha maisha ya wananchi
kwa ajili tu ya njaa yake, ujue ana upungufu na hafai,”alisema.
Katika hatua nyingine, Mohamed alisema Serikali ya Zanzibar,
imeridhishwa na hatua ya ATCL kuanza kulipa deni la sh. milioni 241 la viwanja
vya ndege Zanzibar, kwa kuwa itawezesha ufanisi katika utendaji.
Salum alihimiza haja ya deni hilo kumalizwa kwa wakati.
Naye, Mwenyekiti wa kamati
hiyo, Hamza Hasan Juma, alisema shirika
hilo limepita katika changamoto nyingi na hatua ya Rais Dk. Magufuli, kwa nia
moja, kufanya maboresho ni lazima wasio na mapenzi na taifa waumie na kulitakia
mabaya.
Alisema hatua iliyopo ATCL katika kwenda kwenye ushindani wa
biashara inajieleza, hivyo ni lazima
kufufuka kwake kutawauma na kuwaudhi wengi.
"Lilivyokufa hakuna aliyekuwa analisemea, sasa
linafanyakazi vizuri ni lazima liwaudhi na kulisemea vibaya na hii iwe tija kwa
watendaji kufanya kazi,"alisema.
Aliutaka uongozi wa ATCL, kuona haja ya kuwa na wajumbe wa
bodi na kurugenzi yenye kuzingatia sheria, kwa kuwapo na watendaji kutoka
Zanzibar na kumaliza changamoto ya marubani iliyopo.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo , Mwakilishi
wa Chakechake, Suleiman Sarahan , alisema
ni vizuri shirika hilo kumtosikiliza mtu na kwendau taratibu na kwa safari
yenye uhakika, kuliko kukimbia huku likiisababishia Taifa hasara.
Sarahan alisema mtikisiko wa kisiasa nchini ni jambo la
kawaida, muhimu wasifikie kwenye vita kwa kuwa wapinzani hupinga kila kitu kwa
kuwa ndio ulaji wao.
"Wapinzani hawana jema, kupinga kwao ni ulaji, tuangalie
ATCL inafanya nini na ipo hatua gani, hakuna muda wa kubishana
nao,"alisema.
Alisema ipo haja ya kuboresha mishahara kwa watendaji,
hususani marubani ili kuchochea ufanisi wa kazi na kuwa na wigo wa soko la nje
ya nchi.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Mhandisi Edwin Ngonyani, alisema serikali imejidhatiti kuwa na
mabadiliko katika shirika hilo.
"Hii ni ATCL mpya, hatutampa nafasi mtoto wa mjomba wala
shangazi, tunataka utendaji bila kurudi nyuma, nawahakikishia tutaendelea
kufanya vizuri,"alisema
Mwenyekiti wa Bodi, Mhandisi Emanuel Korroso, alisema pamoja
na kukamilika kwa ununuzi wa ndege
mbili za Bombadier Q400, zilizoanza kazi, ndege nyingine iliyotarajiwa kuwasili
Julai, mwaka huu, itaingia nchini, muda si mrefu.
Alisema lengo la shirika hilo ni kutoa huduma bora ndani na
nje ya nchi, ambapo nchini Comoro, zinafanya vizuri na matarajio ni kuanza
safari za Nairobi, Entebe na Bunjumbura.
Mhandisi Ngonyani alisema mfumo mpya wa utoaji huduma katika
ukatishaji tiketi na udhibiti wa mapato, utasaidia kufikia lengo katika mpango wa miaka mitano,
huku likitarajia ujio wa ndege mpya mbili CC 300, zenye uwezo wa kubeba abiria
132, ambazo zitawasili nchini June 2018.
Pia, alisema ndege moja ya masafa marefu aina ya Boeing 787,
yenye kubeba abiria 262, itawasili Julai, 2018, huku ununuzi wa ndege hiyo
ukizingatia bajeti ya mwaka ujao wa fedha.
No comments:
Post a Comment