BODI ya Utalii Tanzania (TTB), imeridhishwa na idadi wa ya
watalii kutoka China na kusema kuwa,
endapo kutakuwa na safari za ndege za moja kwa moja, itasaidia kupunguza
gharama za safari na kuchochea utalii.
Mwenyekiti wa Bodi ya TTB, Jaji mstaafu Thomas Mihayo, alisema
hayo juzi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa.
Alisema endapo kutakuwa
na ndege ya moja kwa moja kutoka Tanzania mpaka China, idadi kubwa ya watilii
kutoka nchi hiyo itaongezeka na pia
mataifa mengine, hivyo sekta ya utalii itachangia zaidi mapato
ya serikali.
Jaji mstaafu Mihayo alsiema hayo baada ya kumaliza ziara ya
kuwatembeza waandishi waandamizi wa habari kutoka China, katika Hifadhi za
Ngorongoro Crater na Manyara.
Alisema vivutio vya utalii vilivyopo nchini ni tunu kubwa kwa taifa na pia
vinawaleta watalii kutoka sehemu mbalimbali.
“Ujio wa wanahabari hawa ni fursa kwetu kwani watakwenda kuwa
mabalozi wazuri kwa kutoa machapisho na habari nchini kwao, kuhusu vivutio vya utalii vilivyoko Tanzania,”
alisema.
Kwa mujibu Jaji mstaafu Mihayo, waandishi hao kutoka China,
wameonyesha nia ya dhati ya kuvitangaza vivutio nchini, hivyo kutokana na urafiki wa kihistoria uliopo
kati ya China na Tanzania, mpango huo utakuwa na mafanikio makubwa.
Alisema China ni nchi yenye watu wengi duniani, hivyo kupitia
waandishi hao, watawafikia wananchi wengi wa nchi hiyo kwa kuandika makala na
machapisho mbalimbali, kuhusiana na vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
“Changamoto kubwa waliyoiona ni gharama ya usafari wa ndege kuwa
ni kubwa kutokana na kutokuwepo kwa ndege za moja kwa moja,” alisema.
Mwenyekiti wa bodi hiyo alisema usafiri wa anga utakapoimarishwa, utachochea
idadi kubwa ya watalii kutoka China.
Alisema tayari Rais Dk. John Magufuli, ameahidi kuleta ndege
kubwa itakayofanya safari ndefu, hivyo itasaidia kupata soko la watalii kutoka China
na kuongeza mapato.
Jaji mstaafu Mihayo alisema halmashauri na wawekezaji katika
hoteli zilizopo katika maeneo ya vivutio vya utalii, waunganishe nguvu ili
kutatua changamoto za barabara kwani zimekuwa kero kwa wageni.
Alisema miundombinu ya barabara kwenda maeneo ya hoteli katika
vivutio ni mibovu , hivyo serikali kwa kushirikiana
na sekta binafsi, wajipange kuiboresha ili iwe rafiki na kuvutia watalii zaidi.
Akizungumza kwa niaba ya watalii wengine, Mhariri Msaidizi kutoka China Daily Media
Group, Kang Bing, alisema wamefurahi kuona vivutio vilivyopo nchini na ukarimu
wa Watanzania.
“Tulitembelea maeneo mbalimbali kama Ngorongoro na Ziwa
Manyara na kuona wanyama na ndege, mandhari nzuri na hili limekuwa somo jipya
kwetu,” alisema.
Alisema watakwenda kuwa mabalozi wa kutangaza maeneo ya vivutio vya utalii
kupitia machapisho na makala mbalimbali, ili kuchochea idadi ya watalii kutoka
China kuongezeka.
Waandishi sita kutoka Beijing Press Group, China Daily,
International Liaison Department, English News Service na China Radio
International, walitembelea Hifadhi ya Ziwa Manyara na Ngorongoro Crater.
No comments:
Post a Comment