Tuesday, 22 August 2017
MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI KUHAKIKIWA
SERIKALI imesema imeanza uhakiki wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), ili kuyagundua yale ambayo hayajasajiliwa kwa lengo la kuyafuta.
Kauli hiyo ilitolewa juzi, mjini hapa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Sihaba Nkinga, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Sihaba alisema mashirikia, ambayo yatagundulika hayajasajiliwa, yatafutwa mara moja na kwamba, uhakiki huo utafanyika nchi nzima .
“Tutazifuta NGOs ambazo hazijasajiliwa na uhakiki huo ulishaanza tangu Agosti 21 na utamalizika Septemba 4, mwaka huu,’’ alisema.
Sihaba alisema wizara itafanya tathmini ya mwenendo wa uhakiki katika kanda zote na kutoa uamuzi stahiki ili kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafanikiwa na haimuonea mtu.
“Isipokuwa ni lazima niseme kuwa, hizo NGOs ambazo zitabainika hazijasajiliwa, tutazifuta katika rejesta ya NGOs na hazitaruhusiwa kufanya shughuli zao hapa nchini,’’alisisitiza.
Aidha, Sihaba alisema kuanzia Agosti 21 hadi Novemba 3, mwaka huu, usajili wa NGOs mpya utasimamishwa ili kutoa fursa kwa wataalamu kuchakata kikamilifu taarifa kutoka vituoni.
Alisema zoezi hilo litafanyika katika kanda tano, ambazo ni mashariki,
itakayojumuisha mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Morogoro na Dar es Salaam, ambapo kituo kitakuwa Dar es Salaam.
Alizitaja kanda zingine kuwa ni ya kati, ambayo itajumuisha mikoa ya Dodoma, Tabora na Singida, ambapo kituo kitakuwa Dodoma.
Kanda nyingine ni ya Ziwa, ambayo itakuwa na mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Mara na Mwanza, ambapo kituo kitakuwa Mwanza.
Pia, alisema kutakuwa na kanda ya Kaskazini, ambayo itakuwa na mikoa ya Kilimanjaro, Manyara, Arusha na Tanga, ambapo kituo kitakuwa Kilimanjaro.
Aliitaja kanda nyingine kuwa ni nyanda za juu, ambayo itahudumia mikoa ya Katavi, Rukwa, Ruvuma, Njombe, Iringa na Mbeya, ambapo kituo kitakuwa Mbeya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment