Thursday, 24 August 2017
POLISI WAPEKUA NYUMBANI KWA TUNDU LISSU
POLISI Kanda Maalumu Dar es Salaam, wamefanya upekuzi kwa saa tatu, nyumbani kwa Mbunge Tundu Lissu (Singida Mashariki- CHADEMA), iliyoko eneo la Tegeta, Dar es Salaam.
Lissu, alikamatwa na polisi juzi, baada ya gari lake kuzingirwa mbele na nyuma, akiwa anatoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mwanasheria huyo wa CHADEMA, alitiwa mbaroni saa 7.15 mchana, muda mfupi baada ya kutoka mahakamani hapo, alikokuwa akimtetea mshitakiwa Yericko Nyerere.
Taarifa iliyotolewa na wakili wake, Fred Kihwelo, jana, ilisema Lissu alipelekwa kukaguliwa nyumbani kwake saa 5 hadi 7 mchana, akiwa ameambatana na polisi sita.
Alisema lengo la ukaguzi huo lilikuwa kutafuta taarifa, ambazo alizitoa kwenye mkutano wa waandishi wa habari, uliofanyika wiki iliyopita, kuhusiana na ndege za serikali kuzuiwa Canada.
Kihwelo alisema baada ya ukaguzi huo, hakuna taarifa yoyote waliyoikuta nyumbani kwa Lissu na kuamua kurudi Kituo Kikuu cha Polisi, saa nane mchana.
"Tunachohangaikia ni Lissu kupelekwa mahakamani au apewe dhamana, lakini ikifika kesho (leo), mteja wetu hajapewa dhamana, tutapeleka kesi Mahakama Kuu kwa ajili ya kuomba dhamana kwa sababu muda wa kukaa ndani wa saa 24 umepita," alisema wakili huyo.
Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya, alisema hana taarifa ya kushikiliwa kwa mbunge huyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment