Thursday, 24 August 2017

UINGEREZA YAMWAGA TRILIONI MOJA MIRADI YA MAENDELEO


SERIKALI ya Uingereza imetoa Dola za Marekani milioni 450 (sawa na sh. trilioni moja), kwa ajili ya kusaidia miradi ya maendeleo nchini.

Msaada huo ulitangazwa jana na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Maendeleo ya Kimataifa na Masuala ya Afrika katika Ofisi ya Mambo ya Nje na Jumuia ya Madola ya Uingereza, Rory Stewart, alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Dk. Magufuli, Ikulu, Dar es Salaam.

Stewart alisema fedha hizo zitaelekezwa katika maeneo mbalimbali ya maendeleo, hususan kuinua ubora wa elimu na kuongeza idadi ya watoto wanaopata elimu na kuimarisha miundombinu, hususan barabara na bandari.

Aliyataja maeneo mengine kuwa ni kuinua kilimo cha kibiashara na viwanda, vikiwemo vya pamba na nyama.

Waziri huyo alimpongeza Rais Dk. Magufuli kwa kazi kubwa iliyofanywa na serikali katika mapambano dhidi ya rushwa na hatua zinazochukuliwa kuimarisha elimu kwa kuwapa nafasi Watanzania wengi zaidi kupata elimu.

“Nilitembelea shule moja hapa Dar es Salaam, jana, nimejionea jinsi sera ya kutoa elimu bila malipo ilivyoleta mabadiliko makubwa katika kuongeza idadi ya wanafunzi.

"Nimezunguukia shule, nimezungumza na wazazi, walimu, idadi ya wanafunzi imeongezeka karibu mara mbili, hili ni jambo kubwa sana kutokea kwa muda mfupi na linaleta mabadiliko makubwa. Katika maisha ya watu, elimu ni kila kitu,”alisema.

Alibainisha kuwa, wananchi wa Uingereza wanaipenda Tanzania na serikali yao inaendelea kushirikiana nayo katika masuala mbalimbali ya uhusiano, ushirikiano na kwamba, ana matumaini kuwa msaada ilioutoa utasaidia kuinua uchumi na maisha ya Watanzania.

Kwa upande wake, Rais Dk. Magufuli alimshukuru Waziri Stewart kwa kuja nchini na kumuomba amfikishie shukrani zake kwa Malkia Elizabeth II na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Theresa May, kwa msaada mkubwa uliotolewa kwa lengo la kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na serikali yake.

Rais Magufuli alisema Uingereza ndiyo nchi inayoongoza kwa uwekezaji nchini na alimhakikishia kuwa, Tanzania inatambua mchango mkubwa wa nchi hiyo katika maendeleo yake.

Aliwataka Watanzania kuelewa kuwa, hatua zinazochukuliwa na serikali dhidi ya rushwa, zina manufaa makubwa kwa nchi na kwamba, itahakikisha fedha za msaada zilizotolewa na Uingereza, zinasimamiwa vizuri.

“Ndio maana tunawaomba Watanzania waendelee kutuunga mkono katika mapambano dhidi ya rushwa. Rushwa ni ugonjwa mbaya sana, tukijisafisha katika hili, nchi yetu itakwenda mbele. Kutokana na juhudi tunazozifanya, wapo wengine wanalalamika, lakini matokeo yake ni makubwa na ndio maana ndugu zetu Waingereza wanaona.

“Pia, nitoe wito kwa Watazania kulipa kodi. Hatuwezi siku zote kutegemea fedha zitokanazo na kodi kutoka kwa nchi marafiki kama Uingereza, ni lazima tujenge mazingira ya Watanzania kuamini kuwa, kulipa kodi ni kitu muhimu katika maendeleo yao,”alisisitiza.

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cooke, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Augustine Mahiga, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Doto James.

Katika hatua nyingine, Rais Dk. John Mgufuli, amemteua Luteni Kanali Fredrick Felix Milanzi kuwa Kamishna wa Operesheni wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Dar es Salaam, ilisema Luteni Kanali Milanzi anachukua nafasi ya Mihayo Msikela, ambaye amerejeshwa Makao Makuu ya Polisi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uteuzi huo unaanza mara moja.

Wakati huo huo, Rais Dk. Magufuli, jana, alifanya mazungumzo na Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Rogers Siyanga, ambaye alimuhakikishia kuwa kazi ya kukabiliana na biashara na matumizi ya dawa za kulevya inaendelea vizuri.

Alisema tatizo la dawa za kulevya lilikuwa kubwa, ambapo alitaja dawa za kulevya, ambazo mamlaka yake inapambana nazo kuwa ni bangi, heroine, cocaine na kemikali bashirifu.

Siyanga alisema mamlaka yake kwa sasa imeanza kukamata na kuharibu mashamba ya bangi na bangi iliyovunwa.

Alibainisha kuwa mikakati mitatu inayotumika katika mapambano dhidi ya tatizo hilo ni pamoja na kuzuia dawa za kulevya zisiingie nchini, kutoa elimu kuanzia shule za msingi, sekondari na vyuo na kwenye jamii, ili watu waache kutumia dawa za kulevya.

Pia, alisema mamlaka yake ikishirikiana na taasisi zingine, wanatoa tiba kwa walioathirika na dawa za kulevya, ambapo alitoa wito kwa waaathirika hao kupelekwa kwenye mamlaka hiyo ili watibiwe.

No comments:

Post a Comment