Tuesday, 22 August 2017
MKOJO WA MANJI WAKUTWA NA DAWA ZA KULEVYA
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeelezwa sampuli ya mkojo wa mfanyabiashara Yussuf Manji, ilikutwa na dawa za kulevya baada ya kufanyiwa uchunguzi na ofisi ya mkemia mkuu wa serikali.
Maofisa wa Jeshi la Polisi, Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ramadhani Kingai na D/Koplo Sospeter, wamedai majibu ya mkojo huo, yalitokana na uchunguzi uliokuwa umefanywa na ofisi ya mkemia mkuu wa serikali.
Kingai, ambaye ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Sospeter, walidai hayo jana, mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha, walipokuwa wanatoa ushahidi kwenye kesi ya matumizi ya dawa za kulevya, inayomkabili Manji.
Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, upande wa jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis huku Manji akitetewa na Wakili Hudson Ndusyepo.
Akitoa ushahidi akiwa shahidi wa kwanza wa upande wa jamhuri, Kingai alidai Februari 9, mwaka huu, alikuwepo ofisini kituo kikuu cha polisi kati, ambapo alishughulikia kufanya uchunguzi wa suala lililoripotiwa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, kwa watuhumiwa wanaoshukiwa kutumia dawa za kulevya.
“Siku hiyo nilimpokea mtuhumiwa Manji na Josephat Gwajima. Manji alikuja kuripoti kituoni hapo na alikuja moja kwa moja kwangu. Alipofika kwangu, nikiwa mwenyekiti wa kamati ya uchunguzi wa suala hilo, nilielekeza apelekwe kwa mkemia mkuu akapimwe ili kuweza kujiridhisha kama anatumia dawa za kulevya ama la,” alidai.
Shahidi huyo alidai alimuagiza D/ Koplo Sospeter ampeleke Manji kwa mkemia mkuu kwa sababu tuhuma zilizokuwepo ni kwamba, anatumia dawa za kulevya na anajihusisha na biashara haramu ya dawa hizo.
Kingai alidai agizo hilo lilitekelezwa, ambapo Manji alipelekwa na akiwa mwenyekiti wa kamati ya uchunguzi, baada ya maofisa wa mkemia mkuu kumaliza kufanya uchunguzi, waliwapelekea taarifa kwamba, mtuhumiwa huyo anatumia dawa za kulevya.
Shahidi huyo alidai Gwajima, ambaye alipelekwa siku moja na Manji kwa mkemia mkuu, hakuonekana kutumiwa dawa hizo. Alidai baada ya kupata taarifa, alielekeza mtuhumiwa huyo kufunguliwa jalada la kesi na baadae lilipelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) na hatimaye alifunguliwa mashitaka mahakamani.
Baada ya hapo, shahidi huyo alihojiwa na wakili wa Manji, Ndusyepo na sehemu ya mahojiano hayo ni kama ifuatavyo;
Wakili: Shahidi ulisema ulitoa maelekezo kuwa, Manji apelekwe kwa mkemia mkuu. Una mamlaka yoyote ya kuamuru hivyo?
Shahidi: Ninayo mamlaka na njia sahihi ya kujua iwapo mtuhumiwa anatumia dawa za kulevya ama la, ni kwenda kwa mkemia mkuu.
Wakili: Kwa maelezo yako, ulifanya maombi ya kufanya uchunguzi kwa maandishi au kwa kumtumia Sospeter?
Shahidi: Ofisi yangu iliandaa barua, ikimhitaji mkemia mkuu afanye uchunguzi iwapo Manji anatumia dawa za kulevya ama la.
Wakili: Sheria inakutaka uombe amri ya mahakama, je ulifanya hivyo?
Shahidi: Sijaona kifungu kinachonilazimisha kufanya hivyo na nilifuata utaratibu.
Wakili: Kifungu cha 63 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kinazungumzia nini mtu unayempeleka kumfanyia uchunguzi akiwa chini yako?
Shahidi alipata fursa ya kusoma kifungu hicho cha sheria na kudai kwamba, hakuwa anafanya uchunguzi wa kitabibu.
Wakili: Mkemia alikuwa anafanya nini?
Shahidi: Uchunguzi wa sampuli aliyopelekewa na Manji aligundulika anatumia dawa za kulevya ziitwazo benzodiazepine. Alidai hana ufahamu wowote kuhusu dawa hizo.
Baada ya Wakili Ndusyepo kuuliza maswali hayo, mshitakiwa Manji alimuandikia wakili wake maswali ya kumuuliza shahidi huyo yasemayo:
Wakili: Februari 9, mwaka huu, Manji alikuwepo kituo kikuu cha polisi cha kati, je ulishiriki kumpa dawa?
Shahidi: Hapana.
Wakili: Manji akiwa chini yako na unatoa maelekezo akapimwe kwa mkemia, je, alikubali kufanya hivyo?
Shahidi: Ndio maana hakukubali kwa kuwa tulimweleza akakubali na kupelekwa na Sospeter.
Baada ya kumaliza kutoa ushahidi, alifuata shahidi wa pili, Sospeter, ambaye alidai alimpeleka Manji kwa mkemia mkuu, ambapo alichukuliwa sampuli ya mkojo wake na kufanyiwa uchunguzi.
Sospeter alidai Februari 10, mwaka huu, alikwenda kuchukua majibu, ambayo yalieleza kuwa mkojo wake ulikutwa na chembechembe za dawa za kulevya. Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa leo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment