Tuesday 22 August 2017

WATOA RUSHWA CCM WAFUNGULIWA MAFAILI



CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema hakina mzaha katika kudhibiti vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi wa viongozi wake na kwamba, kimefungua mafaili ya kufuatilia mwenendo wa wagombea nafasi za uongozi ngazi ya mikoa.

Kimesema kimeanza kuweka kumbukumbu katika mafaili ya wagombea hao, hususan maeneo yaliyoanza kutolewa malalamiko na baadhi ya wanachama na wagombea wa nafasi husika.

Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula, alisema hayo jana, alipozungumza na UHURU, kuhusu mwenendo wa uchaguzi wa Chama katika ngazi mbalimbali.

Mangula alisema kamati yake ndogo ya Usalama na Maadili, inaendelea na kazi ya kufuatilia kwa karibu mwenendo wa viongozi wake na atakayekiuka maadili hatateuliwa kuwania nafasi husika.

“Tulikuwa tunafanya tathmini ya uchaguzi wa ngazi za mashina, matawi na kata, ambapo kwa zaidi ya asilimia 90, umefanyika vizuri. Sasa tunafuatilia uchujaji wa wagombea ngazi za wilaya na mkoa.

“Lengo ni kuhakikisha tunapata safu za viongozi bora watakaokiwezesha Chama kupata ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa Rais , wabunge na madiwani 2020,”alisema.

Mangula aliwaonya wagombea wa nafasi za uongozi, wasijaribu kushawishi wapigakura kwa rushwa, badala yake wazingatie kanuni za maadili na miongozo ya uchaguzi ili wawe salama.

“Ikithibitika mtu ametoa rushwa ili achaguliwe katika nafasi fulani, tutafuatilia kikamilifu, uchunguzi utakapokamilika mtuhumiwa ataitwa katika kamati ya usalama na maadili kama kuna ulazima, kabla ya kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni zetu,”alisema.

Alisema pia vikao vitakavyochelea kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa wa makosa hayo, pia vitakuwa vimetenda kosa la kimaadili, hivyo hawatasita kuchukua hatua kwa vikao husika, kwa kuwa lengo ni kujenga Chama chenye nidhamu.

Katika hatua nyingine, Mangula alisema watendaji na wajumbe wa vikao vya uchujaji vitakavyopitisha majina ya wasaliti kugombea uongozi, watajiweka pabaya.

Alisema wapo waliofukuzwa, waliosimamishwa na wengine waliowekwa chini ya uangalizi, hivyo Chama hakihitaji mtu aliyesababisha kipoteze nafasi achaguliwe tena kuwa kiongozi, maana yake ni kuendelea kujimaliza.

“Hatuwezi kupanga watu ili waende kushindwa tena, lazima tupange timu mpya ya ushindi. Kuna baadhi ya viongozi wanawaonea haya, sasa nasema kanuni hazina haya, viongozi tusimamie kanuni.

"Watendaji na vikao vitakavyopitisha majina ya wasaliti kwenye nafasi za uongozi, hawakitakii mema Chama, hivyo na wao hawatakuwa salama, tutatumia kanuni zetu za maadili kutoa adhabu kwa wahusika,”alisema.

Mangula aliwaonya viongozi kutojihusisha na upangaji safu kwa ajili ya kupata watu wa kuwasaidia kwenye uchaguzi mkuu ujao, badala yake wahakikishe wanapata viongozi bora, watakaokiwezesha Chama kushinda uchaguzi.

Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Bara, pia aliwataka watendaji kuhakikisha wanafuata kanuni katika kuteua idadi ya wagombea kulingana na nafasi kwa mujibu wa kanuni.

"Mfano kanuni inasema nafasi moja watu watatu, sasa mtu anaweka wanne, jambo ambalo halikubaliki,"alisisitiza.

Mangula alisema wanapaswa kuzingatia kwamba, mtu mmoja anapaswa kugombea nafasi moja, lakini yapo maeneo mtu mmoja kagombea nafasi zaidi ya moja na vikao vimepitisha.

“ Sijui wanatujaribu au hawajui kanuni, hili nalo tunalifuatilia,” alisema.

Alisema katika eneo hilo, kikao kizima cha uchujaji kinaweza kuadhibiwa, kwa kuwa kitakuwa kumethibitisha kwamba, wote hawatoshi kuwa viongozi.

Baada ya kukamilisha uchaguzi ngazi za mashina, matawi na kata, CCM inaendelea ya vikao vya uchujaji wa nafasi za uongozi wa wilaya kwa jumuiya na Chama, kabla ya uchaguzi utakaofanyika Septemba, mwaka huu.

1 comment:

  1. Stainless Steel Magnets - titanium arts
    Ironing the Stainless Steel ventureberg.com/ Magnets (4-Pack). Made in Germany. The Titanium Arts Stainless Steel https://access777.com/ Magnets mens titanium wedding bands are an alloy made of หารายได้เสริม steel herzamanindir.com/ in stainless steel

    ReplyDelete