Tuesday 22 August 2017

DAKTARI FEKI ALIYENASWA MUHIMBILI ADAKWA AMANA



KIJANA Abdalah Juma, aliyewahi kukamatwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), akidaiwa kujifanya daktari, amenaswa tena katika Hospitali ya Rufani ya Amana, jijini Dar es Salaam, kwa tuhuma hizo hizo.

Juma, alinaswa jana, ndani ya Hospitali ya Amana, nyakati za mchana, akijifanya daktari, baada ya kuwekewa mtego na uongozi wa hospotali hiyo.

Kukamatwa kwa Juma,  kumekuja miezi mitatu, tangu Juni 19,  mwaka huu, alipokamatwa katika Hospitali ya Muhimbili, kwa kujifanya daktari.

Wakati alipokamatwa Muhimbili, kijana huyo alijifanya kutoa huduma katika maabara kuu huku uongozi ukiwa hauna taarifa ya kuwepo kwa huduma aliyokuwa akiitoa, kitu ambacho kilisababisha kushtukiwa na kukamatwa.

Baada ya kukamatwa, uongozi wa hospitali hiyo ulifanya uchunguzi na kubaini kijana huyo hakuwa daktari kama alivyokuwa akijitambulisha na kwamba, alikamatwa baada ya kuwekewa mtego na askari wa hospitali hiyo.

MAMBO YALIVYOKUWA

Daktari wa Kitengo cha Watu wanaoishi na Virusi  vya Ukimwi (WAVIU), Shani Mwaruka, alikiri kukamatwa kwa mtuhumiwa.

Alisema Juma, alinaswa baada ya uongozi kupata malalamiko kutoka kwa watu waliokuwa wakihitaji huduma hospitalini hapo.

“Kuna watu walileta malalamiko kwamba, kuna daktari wa Amana amewaomba fedha ili awape huduma. Tuliamua kufuatilia haraka na leo (jana) ndipo walipokubaliana kukutana hapa hospitali,”alisema  Dk. Mwaruka.

Alisema tayari hospitali hiyo iliweka mtego wa maofisa wake ambapo Juma aliingia bila hofu na kukutana na watu ambao alitaka wampe fedha ili awahudumie ndipo aliponaswa.

“Hili tukio la daktari feki kukamatwa katika hospitali ni la kwanza, ila huyu kijana imebainika aliwahi kukamatwa Muhimbili kwa kujifanya daktari. Kwa maana hiyo ni mtu hatari kwani tuna hofu anaweza kuja kuingia katika vitengo nyeti na hata kuleta maafa,”alifafanua.

Baadhi ya watu waliodaiwa kuombwa fedha na  daktari huyo feki, walisema aliahidi kuwatafutia kazi katika hospitali hiyo.

Mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Cecilia, alisema  Agosti  9, mwaka huu, kijana  huyo aliwaeleza kuwa, kuna kazi katika Hospitali ya Amana na yeye kama daktari bingwa anayefanya kazi hapo, anaweza kuwasaidia.

“Alituambia  fomu zinatolewa katika Hospitali ya Muhimbili kwa malipo ya shilingi 150,000, lakini kwa kuwa wao ni madaktari, atatufanyia kwa shilingi 100,000. Tulichanga fedha hizo na zilifikia shilingi 800,000, tukampatia,”alieza Cecilia.

Aliongeza kuwa Juni 19, mwaka huu, aliwaita katika Hospitali ya Amana  ili kufanyiwa usahili, lakini hakutokea na simu akawa hapokei.

“Tuliamua kuuliza kwa madaktari kama wanamfahamu, lakini hakuna aliyemfahamu, ndipo tulipobaini kwamba, tumetapeliwa na kuamua kufanya mtego kwa kushirikiana na uongozi uliofanikisha kumnasa  leo (jana),”alieleza.

Hata hivyo, mtuhumiwa huyo alikataa kuongea lolote huku akionekana kutojali.

Alikamatwa hospitalini hapo na polisi waliovaa kiraia, ambao walimpeleka Kituo cha Polisi Pangani, wilayani Ilala.

No comments:

Post a Comment