SERIKALI imesema iko tayari kugharamia matibabu ya
Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu, popote duniani pindi
itakapopata maombi kutoka kwa familia yake.
Taarifa ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, iliyosambazwa kwa vyombo vya habari jana, ilieleza
kwamba, mbali ya maombi hayo, serikali pia inasubiri taarifa rasmi kutoka kwa
madaktari wanaomtibu kuhusu mahitaji halisi.
“Akiwa kama Mtanzania na Mbunge, serikali iko
tayari kugharamia matibabu zaidi ya Lissu, popote duniani mpaka apone ili aweze
kuendelea na kazi ya kuwahudumia Watanzania na wana Singida,” ilieleza sehemu
ya taarifa hiyo.
Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu, alisema
kwamba, serikali iko tayati kufanya hivyo, endapo maombi yatawasilishwa rasmi,
ikiwa ni pamoja na kupata maendeleo ya afya yake kutoka kwa madaktari
wanaomhudumia hivi sasa jijini Nairobi, Kenya.
Ummy alisema, anashangazwa na dhana ya
kuchangishana kwa ajili ya matibabu ya Lissu, akatahadharisha kwamba, matapeli
wanaweza kutumia mwanya huo kujipatia fedha.
Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim
Juma, amesema tukio la kushambuliwa Lissu na watu wasiojulikana, ni funzo kwa
namna gani nchi zimejipanga kupambana na uhalifu na kitu cha kwanza ni
kukusanya ushahidi.
Amesema nchi nyingine zimefunga kamera katika
barabara kuu, ambapo Nairobi kumefungwa kamera za CCTV kila sehemu katika
barabara na nyumba, ambao huo ni ushahidi wa kutosha.
Jaji Mkuu Profesa Juma aliyasema hayo jana, jijini
Dar es Salaam, alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na waandishi wa habari juu
ya tamko la Chama cha Mawakili cha Uingereza, kuhusiana na tukio la
kushambuliwa kwa mbunge huyo.
Akizungumzia tamko hilo, Jaji Mkuu alisema kwa
kanuni zao, hawaruhusiwi kutoa maoni wala kuzungumza jambo moja kwa moja,
ambalo litafika mahakamani, ndiyo maana wamekaa kimya.
Kuhusu uhuru wa mahakama nchini, ikilinganishwa na
Kenya, Jaji Mkuu alisema, Tanzania ipo huru na kuwataka Watanzania kuendelea
kujidai na sheria na kuzitumia.
No comments:
Post a Comment