Sunday, 24 September 2017

RAIS DK. SHEIN KAIPAISHA ZANZIBAR-HAMAD


MWANASISA mkongwe nchini, Hamad Rashid Mohammed, amesema hali ya kisiasa visiwani Zanzibar ni nzuri kutokana na uvumilivu, upole, uelewa na maono aliyonayo Rais Dk. Ali Mohammed Shein.

Amesema kisiasa, Tanzania ipo sehemu nzuri na kwamba, Rais Dk. Shein amefanya mambo makubwa yaliyosaidia kudumisha amani na utulivu katika visiwa hivyo na kuimarika siku hadi siku.

Hamad, ambaye ni Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Zanzibar, alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita, alipohojiwa na Uhuru, kuhusu masuala mbalimbali yanayovihusu visiwa hivyo.

Hamad alisema, Dk. Shein ni mtendaji mzuri anayepaswa kuigwa na wengine, ambapo utendaji wake umesaidia uchumi wa Zanzibar kuimarika mara dufu.

Alisema Rais Dk. Shein ni kiongozi mtaratibu, mvumilivu, mwenye maono mapana na muelewa, hali ambayo imesaidia hali ya kisiasa katika visiwa hivyo kuimarika siku hadi siku.

Alisema Dk. Shein anajielekeza kwenye masuala ya maendeleo kwa ajili ya wananchi wa visiwa hivyo na kwamba, chini ya utawala wake, Zanzibar imetoka kutoka asilimia zaidi ya 30 ya utegemezi na kufikia asilimia saba.

Mwanasiasa huyo wa zamani wa CUF, aliongeza kuwa, miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika utawala wa Dk. Shein, ni kupandisha kima cha mshahara kwa wafanyakazi.

“Mheshimiwa rais amepandisha mshahara mara mbili ya mfanyakazi aliokuwa anapata na unalipwa kwa wakati kwa wafanyakazi wote. Hayo ni mafanikio makubwa sana katika utawala wake,” alisema.

Pia, alisema kwa mara ya kwanza, Dk. Shein ameweza kunyanyua mapato ya Zanzibar na kwamba, utawala wake ni wa kupigiwa mfano na kuigwa.

Hamad, alisema katika utawala wa Dk. Shein, Zanzibar inaingia kwenye historia kubwa ya kutengeneza mchele wao wenyewe na kuuza.

Alisema sekta ya kilimo imepata mafanikio makubwa na mwaka jana, walizalisha tani 19,000 za mbunga, ambapo mwaka huu, wamezalisha tani 630,000.

“Hali hii imesabishwa na utulivu wa Rais Dk. Shein na miongozo yake na ahadi aliyoitoa kwa wananchi kwamba, Zanzibar ijitosheleze kwa chakula,” alisema Hamad, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa chama cha ADC.

Alisema awali walikuwa wakiagiza asilimia 80 ya matunda kutoka Tanzania Bara, lakini hivi sasa wanaagizia asilimia 20 na iliyobakia wanazalisha wenyewe.

Kuhusu sekta ya uvuvi, Hamad alisema wamefufua kampuni ya uvuvi na wanatarajia wakati wowote wapate meli mbili mpya za uvuvi ili waweze kuvua wenyewe.

Pia, alisema wamejenga masoko mapya matano, matatu yatakamilika mwisho wa mwezi huu.

“Naamini kabisa hii kampuni ya uvuvi tuliyoianzisha, masoko tuliyojenga na wavuvi tukiwapatia zile boti mpya, ambazo tuliwaahidi tukiwapatia sekta ya uvuvi itatoa mchango mkubwa sana katika pato la taifa,” alisema.

Akizungumzia zao la karafuu, alisema tayari wameanza kujua idadi ya mikarafuu na mashamba na kwamba, zao hilo linahitaji kuendelezwa kwa nguvu kubwa.

“Karafu ndio kitu cha ukombozi, kilicholeta taswira ya Zanzibar ni nini, tunahitaji kuwekeza kwenye karafauu.

“Mwaka huu tunategemea kuwa na mavuno makubwa ya karafuu, ninachoomba ni mambo matatu kwanza, watu waichume karafuu kwani serikali imejitahidi kutoa asilimia 80 ya bei ya dunia, hili ni badiliko kubwa sana,” alisema na kuwataka wananchi kupiga vita magendo na kutoikata mikarafuu hovyo.

No comments:

Post a Comment