Sunday, 24 September 2017

MWANAMKE MBARONI KWA KUKUTWA NA KETE 969 ZA COCAINE



POLISI Mkoa wa Kusini Pemba, wamemkamata mwanamke, akiwa na kete 969, zinazosadikiwa kuwa ni dawa za kulevya, zilizokuwa zimehifadhiwa ndani ya DVD.

Mwanamke huyo, aliyekuwa ameongozana na wanaume wawili, alikamatwa katika maeneo ya Baraza la Kiuchumi Zanzibar (PBZ), Chake Chake. Anakuwa mwanamke wa pili kukamatwa ndani ya wiki mbili.

Taarifa zinaeleza kuwa, Septemba 9, mwaka huu, Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, maeneo ya mkoani Pemba, walifanikiwa kumkamata Zuhura Ahmed Ali (29), akiwa na kete 3,621, ambapo alifikiswa mahakamani kwa mara ya kwanza Septemba 14, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari, ofisini kwake, mwishoni mwa wiki iliyopita, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Shikhan Mohamed Shikhan, alimtaja mwanamke huyo  kuwa ni Asha Mohamed Issa (30), mkazi wa Wawi, Chake Chake, huku wenzake wakiwa ni Ali Nyoro Tirima (32) wa Wawi na Salim Said Kombo (23), mkazi wa Konde, Wilaya ya Micheweni.

Pia, Kamanda Shikhan alisema, polisi mkoani humo, tayari inayo majina ya mabaharia wanaofanya kazi katika meli zinazotoka Unguja kwenda Pemba, wanaotumiwa kusafirisha dawa za kulevya.

“Wito wangu kwa mabaharia wa meli zinazotoka Unguja kuja Pemba, tayari tunayo majina  ya meli zote, ambazo wanatoa msaada mkubwa kwa waleta dawa za kulevya, zinapita katika mikono yao, tunawajua na tunawafuatilia kwa karibu,”alieleza.

Vilevile, aliwataka wamiliki wa kampuni za usafiri wa meli, kuwatahadharisha mabaharia wao, kuacha kutumiwa na wahalifu wa bangi na unga.

Kwa upande mwengine, Kamanda Shekhan amewaonya wanawake wanaojiingiza kufanya biashara za dawa za kulevya, kuacha kabisa biashara hizo na kutafuta njia halali za kujipatia kipato.

“Kweli huyu ni mwanamke wa pili kumkamata kwa mkoa wetu, lakini natoa wito kwa wanawake, hiyo siyo biashara ya kusema wanaweza wakapata utajiri, warudi nyuma, watafute biashara zinazokwenda na maadili ya biashara,”alieleza.

No comments:

Post a Comment