Wednesday 30 March 2016

JPM, ATOA KALI YA MWAKA, APIGA MSOSI WA MCHANA MGAHAWANI MWANZA





RAIS Dk. John Magufuli  ameandika historia nyingine ya aina yake katika uongozi wake, baada ya kuamua kula chakula cha mchana katika moja ya migahawa iliyoko pembeni ya uwanja wa ndege wa Mwanza.
Tukio hilo lilitokea jana mchana, wakati Rais Magufuli na mkewe, Janet Magufuli, walipotua kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza, akiwa njiani kwenda nyumbani kwake Chato kwa mapumziko.
Rais Magufuli alipokewa na viongozi mbalimbali wa serikali wa mkoa wa Mwanza, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, Meya wa Jiji la Mwanza, Mstahiki James Bwire, Meya wa Ilemela, Mstahiki Renatus Mulunga na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa, Anthony Diallo.
Akizungumza na viongozi hao pamoja na waandishi wa habari na viongozi wa dini, Rais Magufuli aliagiza kufunguliwa kwa barabara ya Airpot-Igombe hadi Kayenze, iliyofungwa tangu mwaka 2014, kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa kisasa wa Mwanza.
Kufungwa kwa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita saba, kumesababisha usumbufu kwa wananchi wa jiji la Mwanza na vitongoji vyake, vikiwemo vya wilaya ya Ilemela na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliokuwa wakiitumia.
Rais Magufuli alisema kufungwa kwa barabara hiyo kumeleta adha kubwa kwa wananchi wa jiji hilo la kibiashara.
“Natambua lipo suala linalowaumiza wananchi la kufungwa kwa barabara hii ya Airpot-Igombe. Sasa naagiza mkuu wa mkoa kuanzia leo, barabara hii ifunguliwe ili wananchi waitumie ili kuondoa usumbufu wa kuzunguka kupitia Nyakato hadi maeneo ya TX Kata ya Bugogwa, Igombe hadi Kayenze katika kata ya Sangabuye,” alisema.
Rais Magufuli alieleza kuwa serikali itaangalia uwezekano wa kupanua uwanja huo kuelekea mashariki ili barabara hiyo inayopita pembezoni mwa Ziwa Victoria na uwanja wa ndege, iboreshwe kwa kiwango cha lami na kuharakisha maendeleo ya wananchi wa maeneo hayo.
“Katika bajeti ya fedha ya mwaka 2016/2017, tumepanga kutoa fedha kwa lengo la kuhakikisha ujenzi wa uwanja huu unaoboreshwa kuwa wa kisasa na ukamilike ili kuwezesha ndege kubwa kutua kwa wingi na pia kutumiwa kimataifa na nchi za Maziwa Makuu kama tulivyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2015,” alisema.
Alisisitiza kuwa kamwe hataki kusikia tena uwanja huo umefungwa na kuuagiza uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), kuupanua zaidi kwenda mashariki, ambapo kuna nafasi ya kutosha kuliko kulazimisha kufunga barabara muhimu kwa matumizi ya wananchi.
Hii ni mara ya tatu kwa Rais Magufuli kutoa agizo la kufunguliwa kwa barabara hiyo, ambapo mara ya kwanza ilikuwa alipokuwa Waziri wa Ujenzi na mara ya pili, alipofika ofisi ya CCM mkoani Mwanza kusaka wadhamini wakati wa kuwania kuteuliwa kugombea urais ndani ya CCM.
Wakati wa mchakato wa kuwania urais, alimueleza Katibu wa CCM mkoani hapa, Miraji Mtaturu kuwa, akichaguliwa kuwa rais, atahakikisha barabara hiyo inafunguliwa na kuboreshwa kwa kiwango cha lami ili kuwaondolea adha wananchi wanaoitumia.
Awali, Rais Magufuli aliyetua uwanjani hapo saa 5:15 asubuhi, alikwenda eneo walipokuwa wamesimama watumishi wa uwanjani hapo na kuwasalimia kwa kushikana nao mikono.
Wakati akiongozwa na maofisa wa Idara ya Usalama kwenda chumba cha VIP, alikatiza ghafla na kwenda kwenye mlango wa chumba cha kupumzikia abiria, ambao ulikuwa umefungwa na kuomba ufunguliwe, ambapo alipata fursa ya kusalimiana na abiria.

Kabla ya kuanza safari ya kwenda Chato, Rais Magufuli na mkewe waliamua kupata chakula cha mchana kwenye mgahawa wa Victoria, tukio lililopokelewa kwa mshangao mkubwa na wananchi waliofika uwanjani hapo kumlaki.
Wakati Rais Magufuli, mkewe na viongozi hao wa serikali wakiwa wanapata chakula kwenye mgahawa huo, wananchi hao pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa uwanja wa ndege wa Mwanza, walisimama pembeni ya mgahawa huo wakimpungia mikono.
Mbali na kupata msosi kwenye mgahawa huo, Rais Magufuli aliamua kutoa sh. 100,000 na kuwanunulia soda wananchi waliokuwepo kwenye mgahawa huo pamoja na waandishi wa habari.
Mmoja wa wasimamizi wa mghahawa, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alieleza kufurahishwa kwake na kitendo hicho cha Rais Magufuli, na kuahidi kubadilisha jina la mgahawa wake na kuuita ‘Dk Magufuli Café’ ili kuenzi kufika kwake na kula chakula hapo, ikizingatiwa kuwa ni kiongozi mkubwa wa nchi.
Mara baada ya Rais  Magufuli kuondoka  uwanja wa ndege wa Mwanza kuelekea Chato,  Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,  John Mongela alisema  agizo hilo la Rais litatekelezwa mara moja.
“Mimi na Kamati ya Ulizi na Usalama ya mkoa, wilaya pamoja na uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,  Meneja wa Tanroads mkoa wa Mwanza na viongozi wa CCM wilaya ya Ilemela, tunaongozana  muda huu kwenda  TX Kata ya Bugogwa ili kufikisha ujumbe uliotolewa na Rais Dk Magufuli ili wananchi watumie barabara hii kuanzia sasa,” alisema.

Rais Magufuli alipita Mwanza, akiwa njiani kwenda nyumbani kwake Chato, kwa mapumziko ya siku tano. Baada ya mapumziko hayo, Rais Magufuli anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi Jijini Mwanza.  

No comments:

Post a Comment